Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema kuwa zaidi ya raia 27,000 waliokuwa wanashikiliwa kizuizini nchini Saudi Arabia wamerejeshwa nchini mwao tangu Aprili 2024.
Juhudi za kuwarejesha nyumbani ni sehemu ya mpango mkubwa wa serikali wa kuwarudisha takriban Waethiopia 70,000 waliolazimishwa kuondoka Saudi Arabia.
" Mpango huo unatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya sasa ambayo ni ya tatu inatumia ndege 12 za kila wiki kuwasafirisha watu binafsi kurudi Ethiopia," Nebiyu Tedla, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, alisema.
Ameongeza kuwa baada ya miezi minne ya operesheni, kamati ya kitaifa inayosimamia mchakato wa kuwarejesha raia hao nyumbani, imekamilisha asilimia 35 ya mpango wa kurejea kwa wahamiaji 70,000.
Wengi wa watu hawa wameenda Saudi Arabia kwa ajili ya kutafuta ajira , lakini hawana nyaraka muhimu za kuishi nchini humo.
Kulingana na shirika la Mixed Migration Center, Saudi Arabia inapokea wahamiaji wapatao 750,000 kutoka Ethiopia huku takriban asilimia 60 ambayo ni sawa na watu 450,000 ambao husafiri kwenda Saudi Arabia kupitia njia zisizo halali.
Mnamo Machi 30, 2022, Serikali za Ethiopia na Saudi Arabia zilifikia makubaliano ya kuwarejesha makwao zaidi ya Waethiopia 100,000 waliokuwa wakiishi nchini humo kinyume na utaratibu.