Waziri Mkuu wa Ethiopia anasema watu milioni 34 katika sehemu tofauti ya Ethiopia walijitokeza Jumatatu kupanda miti /Photo / Picha: Germa Mergesa

Ethiopia inasema ilifanikiwa kupanda zaidi ya miti milioni 560 kwa siku moja tu, ambayo ikithibitishwa itakuwa rekodi mpya duniani.

Rekodi ya hapo awali ya nchi ilikuwa miti milioni 350 iliyopandwa kwa siku - jambo ambalo ilifanikisha mnamo Agosti 2019.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed aliongoza kampeni ya upandaji miti sJumatatu katika juhudi za kurejesha misitu nchini humo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katika akaunti yake ya twitter, alisema watu milioni 34 walipanda miti katika zaidi ya hekta 300,000 za ardhi nchi nzima.

Walijumuisha watoto, wazee na watu wenye ulemavu. "Inapendeza sana tunapofanya kazi pamoja kwa mafanikio," alisema.

Ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia ilitumia TRT Afrika picha hii kuonyesha takwimu ya juhudi zao za Jumatatu.

Picha kutoka kwa Ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia 

Umoja wa mataifa unasema kuwa Ethiopia inalenga kurejesha misitu ya nchi hiyo ambayo imepungua kutoka 35% ya ardhi yote mwishoni mwa karne ya 19 hadi karibu 4% katika miaka ya 2000.

Rekodi ya sasa ya dunia ya miti iliyopandwa kwa siku moja inashikiliwa na India baada ya zaidi ya watu 800,000 kupanda miti milioni 50 mwaka 2016 katika jimbo la kaskazini la Uttar Pradesh.

Bado shirika la rekodi ya dunia , Guinness World Record haijatoa taarifa kuhusu rekodi hii ambayo Ethiopia imesema imevunja.

TRT Afrika