Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Taye Atske Selassie ameteuliwa kuwa Rais wa Ethiopia, anachukua nafasi ya Sahle-Work Zewde.
Uteuzi wake na wabunge ulithibitishwa wakati wa kikao chao cha leo, 7 Oktoba 2024 na akaapishwa.
Balozi Taye amekuwa akihuhudumu kama Waziri wa Mambo ya nje tangu Februari 8, 2024.
Kabla ya hiyo alikuwa mwakilishi wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa. Pia aliwahi kuwa mwakilishi wa ubalozi wa Ethiopia Los Angeles na Stockhom, na balozi wa Ethiopia nchini Misri.
Taye, 68, anakuwa rais wa tano tangu Ethiopia ilipopitisha katiba yake ya sasa mwaka 1995. Anaweza kushikilia wadhifa huo kwa muda usiozidi mihula miwili ya miaka sita.
Rais wa Ethiopia ndiye mkuu wa nchi ya Ethiopia. Nafasi hiyo kwa kiasi kikubwa ni ya sherehe tu huku mamlaka ya utendaji yakiwa chini ya Baraza la Mawaziri linaloongozwa na waziri mkuu.
Rais wa kwanza mwanamke Sahle-Work Zewde
Sahle-Work Zewde alikuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Ethiopia . Alizaliwa Februari 1950.
Alikuwa rais wa tano wa Ethiopia kutoka 2018 hadi Oktoba 2024.
Amehudumu sana katiak maswala ya mambo ya nje.
Sahle-Work alihudumu kama Balozi wa Senegal, alipukuwa akishughulikia pia Mali, Cape Verde, Guinea-Bissau, Gambia na Guinea, kutoka 1989 hadi 1993.
Kuanzia 1993 hadi 2002, alikuwa Balozi wa Djibouti na Mwakilishi wa Kudumu kwa Mamlaka ya Kiserikali. kuhusu Maendeleo (IGAD).
Baadaye alihudumu kama Balozi wa Ufaransa, mwakilishi wa Kudumu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) akisimamia Tunisia na Morocco kuanzia 2002 hadi 2006.
Huduma kwa Umoja wa Mataifa
Hadi mwaka wa 2011, Sahle-Work alihudumu kama Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kujenga Amani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mnamo 2011, Ban alimteua Sahle-Work kama Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Nairobi
Mnamo Juni 2018, Katibu Mkuu Antonio Guterres alimteua Sahle-Work kuwa Mwakilishi wake Maalum katika Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika (UNOAU) katika ngazi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Alikuwa mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo na kufikia wakati huu, ilitarajiwa kwamba Sahle-Work alikuwa akijiandaa kustaafu.
Na hapo ndipo waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alimteuwa kama rais wa Ethiopia.
Sahle Worke amehudumu kwa muhula mmoja tu , ingawa angekuwa na nafasi ya kuchukua muhula wa pili.