Ethiopia imeshutumu kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mshauri Maalumu wa Kuzuia Mauaji ya Kiimbari, na kuiita "kutowajibika na kutojali."
Afisa wa Umoja wa Mataifa, Alice Wairimu Nderitu, alikuwa ameonya kuhusu kuwepo kwa sababu za hatari kwa ''mauaji ya halaiki na uhalifu unaohusiana na ukatili'' nchini.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Ujumbe wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa ilisema Addis Ababa "inasikitishwa sana" kwamba Nderitu, aliyekabidhiwa jukumu muhimu la kuzuia mauaji ya halaiki, amechagua kutoa "madai yasiyo na uthibitisho na matamshi ya uchochezi" dhidi ya nchi hiyo.
Mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na waasi wa Tigray yalizuka Novemba 2020, wakati kundi la Tigray People's Liberation Front , TPLF, liliposhambulia kambi za jeshi la shirikisho zilizoko katika eneo la kaskazini.
Lakini uhasama ulipungua baada ya pande hizo mbili kutia saini makubaliano mjini Pretoria na Nairobi mwezi Novemba mwaka jana.
Ilisema ripoti hiyo kwamba Umoja wa Mataifa ulikosa vyanzo sahihi katika uchunguzi wake.
Wito wa kuchukua hatua
"Serikali imedhamiria kuhakikisha utekelezaji kamili wa makubaliano haya (ya amani) (na Chama cha Tigray. ) Ethiopia iko katika hatua za mwisho za kuunda Sera ya Haki ya Mpito ili kuhakikisha uwajibikaji na haki," ilisema taarifa hiyo.
Nderitu alitoa tahadhari kuhusu ongezeko la hatari ya mauaji ya halaiki na uhalifu unaohusiana na ukatili katika maeneo ya Tigray, Amhara, Afar na Oromi nchini Ethiopia.
"Ripoti za tukio tunazoziona zilizotoka Ethiopia zinasumbua sana na zinatoa wito wa kuchukua hatua," alisema.
"Ninataka kuelekeza hisia za jumuiya ya kimataifa katika kuendelea kuwepo kwa sababu za hatari kwa mauaji ya kiimbari na uhalifu unaohusiana na ukatili nchini," afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alisema.
Nderitu aliongeza kusema kuwa kuna ripoti inayoonyesha kuuawa kwa familia nzima na wanafamilia walilazimika kushuhudia mauaji hayo dhidi ya wapendwa wao, huku jamii nzima ikifukuzwa katika makazi yao.
Mzozo wa Tigray unaripotiwa kuuwa maelfu huku mamilioni ya watu wakihama makazi yao tangu Novemba 2020.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana iliweka idadi ya watu waliokimbia makazi yao kuwa milioni 2.75, huku watoto milioni 12.5 wakisemekana kuhitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.