Mamlaka ya Mawasiliano ya Ethiopia (ECA) imetangaza kuongeza muda wa siku 20 kwa ajili ya kuwasilisha maombi ya kufuzu (RFQ) kwa ajili ya leseni ya pili ya huduma kamili ya mawasiliano ya nchi nzima inayotolewa macho na nchi kadhaa.
"Tarehe ya makampuni ya kigeni kuwasilisha maombi ilipangwa kuwa Septemba 15, 2023. Hata hivyo, ECA ilionyesha wasiwasi na maombi kutoka kwa wawekezaji kadhaa watarajiwa walioomba kuongezewa muda muda na mamlaka ilikubaliana kikamilifu na ombi hilo," Mamlaka hiyo ilisema katika taarifa yake.
Tarehe ya mwisho ya makampuni kuwasilisha maombi yao rasmi imesogezwa hadi tarehe Oktoba, 6 mwaka huu.
Hadi Mei mwaka 2021, Ethiopia ilikuwa na kampuni moja tu ya mawasiliano ya simu, Ethiotelecom ambayo inamilikiwa na serikali.
Uamuzi wa kufungua sekta ya mawasiliano kwa wawekezaji wa kigeni ulitolewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed alipoingia madarakani mwaka wa 2018.
Waziri Mkuu alidai kuwa ni lazima kuwe na mashindano ya kibisahara ili wananchi wapate huduma bora.
Kukaribisha wawekezaji wa kigeni
Ethiopia ilifungua nafasi tatu za leseni za kampuni ya mawasiliano za kigeni.
Mbili zingechukuliwa na makampuni ya kigeni kwa asili mia moja, na leseni ya tatu ingehusisha kampuni kununua asili mia 45 ya hisa katika kampuni ya taifa ya Ethio telecom.
Mnamo Mei 2021, Safaricom Ethiopia iliibuka kama huduma ya pili ya mawasiliano ya simu nchini humo baada ya kampuni hiyo yenye asili yake nchini Kenya kutoa zabuni ya dola milioni 850.
Mbali na kuipa kampuni ya Safaricom Ethiopia leseni, serikali ya Ethiopia pia ilipa masharti ya kuwekeza dola bilioni 8.5 ndani miaka kumi.
Kuhairishwa kwa kutolewa leseni ya pili kumechangiwa kwa upande mmoja na vita ambavyo vilikumba kaskazini mwa Ethiopia kwa miaka miwili tangu Novemba 2020.
Wataalam wa uchumi wanaelezea kuwa wawekezaji ambao walikuwa na nia ya kugombea leseni ya pili ya mawasiliano katika nchi hiyo yenye soko ya kuvutia yenye watu zaidi ya milioni 11, walihofia kuwa mazingira ya uwekezaji hayakuwa salama.
Kwa sasa serikali inakazana kurudisha imani kwa wawekezaji baada ya kutia saini makubaliano ya amani na kikundi cha Tigray People's Liberataion Front ambacho ilikuwa inavutana nayo kaskazini mwa nchi.
Hivyo inaamini kwamba, wawekezaji ambao wallikuwa wamevutiwa kuwekeza katika sekta ya mawasiliano hivi sasa watakuwa na imani kwamba uwekezaji wao utakuwa katika mazingira salama.