Uongozi wa idara Kuu ya hali ya dharura ya Ethiopia, inasema kuwa juhudi za kurejesha amani ndani ya muda mfupi katika Mkoa wa Amhara zinaendelea kwa lengo la kukamilisha shughuli za utekelezaji wa sheria zinazofanyika katika eneo hilo.
Kambi ya Idara Kuu, iliyoanzishwa ili kutekeleza tangazo la hali ya hatari lililotolewa na Baraza la Mawaziri wiki iliyopita, tayari imebuni viwango vinne vya utoaji amri na idara nne ili kuleta amani.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi na Usalama, anayesimamia idara hiyo, Temesgen Tiruneh, uvunjifu wa amani wa kupangwa uliosababishwa na vikundi vya majambazi umepelekea matatizo ya kiuchumi, kijamii na kiutawala.
Aidha, Tiruneh ameongeza kuwa makundi hayo yamekwamisha shughuli za taasisi zinazotoa huduma za umma, na kuwatorosha wahalifu kwa kuvunja magereza katika baadhi ya maeneo. Vilevile, vitendo hivyo vimekwaza shughuli za kilimo za msimu wa Meher na kuwazuia raia kutembea kwa uhuru au kupata huduma katika mkoa huo, Temesgen aliongeza.
Alisema serikali inaamini kwa dhati kwamba madai yoyote yanapaswa kushughulikiwa kwa njia ya amani na kuwa ilidhihirisha hilo kivitendo hapo awali, na kuongeza kuwa wanahusika kutatua matatizo ya kiusalama katika eneo hilo.
Ingawa hali hiyo ya hatari itakayosalia kutekelezwa kwa miezi sita ijayo, inaweza kukomeshwa kabla ya muda wa kuisha ikiwa Baraza la wawakilishi wa watu litaamua hivyo, idara hiyo pia ina mamlaka ya kutangaza amri ya kutotoka nje, kufunga barabara kwa kipindi fulani, na kufunga au kusitisha huduma za usafiri.
Haya yote yanaendelea huku Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed akimpokea Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir aliyewasili nchini Ethiopia kwa ziara ya kikazi ya siku moja.