Jaribio la Ethiopia la kujiunga tena na Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika (AGOA) kwa mara nyingine halijakamilika huku Ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani (USTR) akiendelea kuiweka Ethiopia katika orodha ya nchi zilizosimamishwa katika tangazo lake la tarehe 21 Disemba.
AGOA ni mpango wa biashara kati ya Marekani na baadhi ya mataifa Kusini mwa Jangwa la Sahara, unaowezesha kufutwa kwa kodi kwa bidhaa zinazouzwa.
Mpango huo ulianzishwa mwaka 2000, kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi hizo kupitia biashara.
Tangazo hilo lilithibitisha kwamba orodha ya nchi za Kiafrika zinazostahiki kuwepo chini ya mpango wa AGOA itasalia bila kubadilika kwa mwaka ujao wa fedha, na kuhifadhi manufaa ya mkataba huo kwa nchi 32 za Afrika zinazostahiki.
Rais Joe Biden wa Marekani alipitisha kuiondoa Ethiopia kutoka AGOA Novemba 2021 kufuatia kuongezeka kwa vita, vilivyoanza mwaka mmoja mapema Novemba 2020, kaskazini mwa nchi. Marekani iliilaumu Ethiopia kwa "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu zinazotambulika kimataifa."
Licha ya majadiliano ya maafisa wa biashara wa Marekani mwezi Julai kuchunguza uwezekano wa marekebisho ya uamuzi wa AGOA, uamuzi wa hivi punde unaifanya Ethiopia kubaki nje ya mfumo huo wa biashara.
Juhudi za mara kwa mara za Ethiopia kurejesha ustahiki wa AGOA bado hazijafaulu, na kuashiria kikwazo chengine katika jitihada zake za kujiunga tena na mpango huo wa kimataifa wa biashara.
Uamuzi huo umesababisha makampuni kadhaa ya kigeni yanayofanya uzalishaji katika eneo la viwanda nchini Ethiopia kufunga biashara na kuondoka Ethiopia baada ya nchi hiyo kuondolewa katika orodha ya AGOA.
Nchi nyengine zabaki nje ya AGOA
Nchi nyengine zilizopigwa marufuku ni pamoja na Uganda, Burundi, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Equatorial Guinea, Eritrea, Gabon na Guinea.
Marekani ilitangaza kuiondoa Uganda kwenye utaratibu wa kunufaika na AGOA kuanzia Januari 2024, baada ya nchi hiyo kupitisha sheria dhidi ya mapenzi ya jinsia moja Mei mwaka huu.
Mali, Niger, Sudan, Sudan Kusini na Zimbabwe pia bado zimebaki nje ya AGOA.