Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia./ Picha: Getty Images

Ethiopia imekaribisha mwaka mpya wa 2016 huku akiidhimisha sherehe za mwaka mpya kwa njia mbalimbali.

Waethiopia kote ulimwenguni wanasherehekea mwanzo wa Mwaka Mpya Wa Ethiopia, 2016 ambao huinguia terehe 11 au 12 Septemba kulingana na mwaka.

Tofauti na sehemu zingine ulimwenguni, kila mwezi katika kalenda ya Ethiopia ina siku 30 huku kalenda hiyo ya Ethiopia ikiwa na miezi 13. Mwezi wa 13 huwa na siku siku 5 au 6.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed na mke wake Zinash Tayachew waliungana na raia wa Ethiopia katika sherehe za kuupokea mwaka mpya huku wakishiriki kwenye ugawanyaji wa chakula kwa wanyonge walioalikwa Ikulu.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed na mke wake Zinash Tayachew washiriki kwenye ugawi wa chakula kwa wanyonge katika ikulu kwa mwaka mpya. Picha: Waziri Mkuu Ethiopia

"Kwa neema ya Mwenyezi Mungu tumevuka 2015 na kuingia enzi mpya. Tumefika hapa kwa sababu tuna chaguo lenye nguvu, watu wenye nguvu na Mola asiyeshindwa. Mafanikio yetu yote yametokana na juhudi za umoja wetu wa kitaifa." Taarifa ya Waziri Mkuu Abiy ilisema.

"Mwaka ujao, tutapunguza changamoto zetu; tutaimarisha umoja wetu wa kitaifa na kuimarisha amani na usalama wa Ethiopia kwa msingi thabiti. Tutainua maendeleo ya Ethiopia kwa kiwango kinachostahili." Abiy aliandika.

Rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde naye ametuma ujumbe wake wa mwaka mpya Kwa Waethiopia wote.

"Makubaliano ya kitaifa yanapaswa kupatikana kupitia majadiliano na mashauriano, na ni jukumu la wote kueneza upendo na maelewano kwa watu na kuzuia chuki." Rais alisema.

Aidha, Mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika AU Moussa Faki Mahamat amewaongoza wakuu mbalimbali katika kuipongeza Ethiopia.

"Melkam Addis Amet! Nawatakia mwaka mpya uliobarikiwa, na uliojaa amani na ustawi kwa dada zetu wote, ndugu, wenzangu, na marafiki wanaosherehekea, " Mwenyekiti aliandika kwenye mtandao wa X.

Wanadiplomasia na viongozi wa nchi mbalimbali nao wamekuwa wakitoa ujumbe wa kuitakia Ethiopia mwaka mpya kwa Waethiopia huku wakiadhimisha Mwaka Mpya.

TRT Afrika