Ujumbe wa Ethiopia uliongozwa na Waziri wa Ulinzi Aisha Mohammed Musse na walifanya mktano na  Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Abdulkadir Mohamed Nur Jama / Picha: Ethiopia Wizara ya Mambo ya Nje.

Ethiopia na Somalia zimekubaliana kufanya kazi pamoja katika kikosi cha kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Hii inafuatia ziara nchini Somalia ambapo ujumbe huo wa Ethiopia umeongozwa na Waziri wa Ulinzi Aisha Mohammed Musse na Waziri wa Mambo ya Nje Mesganu Arga katika ziara ya kikazi nchini Somalia.

Pia walikutana na Waziri wa Ulinzi wa Somalia, Abdulkadir Mohamed Nur Jama .

Hii ni ziara ya kwanza baina ya nchi hizo mbili tangu uhusiano kati ya majirani hao wawili kuvunjika mwaka mmoja uliopita kuhusu mpango wa Ethiopia wa kujenga kituo cha jeshi la majini katika eneo lililojitenga la Somalia.

''Nchi hizo mbili zimekubaliana kushirikiana katika ujumbe wa AUSSOM na kuimarisha uhusiano wa pande mbili,'' Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia ilisema katika taarifa yake siku ya Ijumaa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita liliidhinisha kikosi cha Umoja wa Afrika wa kuleta utulivu na msaada nchini Somalia - unaojulikana kama AUSSOM - kuchukua nafasi ya operesheni kubwa ya AU ya kupambana na ugaidi kuanzia Januari 1, 2025.

Ujumbe wa Somalia ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi, Ali Mohamed Omar, ulitembelea Ethiopia wiki iliyopita na kufanya mazungumzo na Balozi Mesganu Arga, na kuimarisha ushirikiano unaoendelea kati ya nchi hizo mbili.

Kuhamisha majukumu

Wanachama 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama walipiga kura kuunga mkono azimio hilo.

Marekani haikupiga kura.

"Kura hiyo inaashiria hatua zaidi katika kuhamisha majukumu ya usalama wa kitaifa kwa vikosi vya Somalia yenyewe," Baraza lilisema katika taarifa.

Inawaidhinisha wanachama wa Umoja wa Afrika kuchukua hatua zote zinazohitajika kwa muda wa miezi 12, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono serikali ya Somalia, katika kuwaangamiza Al-Shabaab na kundi la Daesh.

Muda wa Kikosi cha sasa cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) ulimalizika Disemba 31.

TRT Afrika