Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud aliwasili Ethiopia Jumamosi kwa ziara yake ya kwanza rasmi tangu mazungumzo ya upatanishi ya Uturuki kutatua mizozo ya muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alimkaribisha Mohamud kwa mapokezi ya hali ya juu, na viongozi hao wawili walifanya majadiliano yaliyojikita katika kuimarisha uhusiano na kushughulikia vipaumbele vya pande zote, kulingana na chapisho la Ahmed kwenye X.

"Ziara hii inatokana na makubaliano ya hivi majuzi yaliyofikiwa Ankara. Ushirikiano huu mpya unasisitiza enzi mpya ya ushirikiano kati ya Somalia na Ethiopia," ilisema taarifa kutoka kwa Urais wa Somalia, Villa Somalia.

Walichokubaliana

Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili ''yalizingatia haja ya kuendelea na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama wa nchi hizo mbili,'' kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa majadiliano yao.

''Walikubali kurejesha na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili kupitia uwakilishi kamili wa kidiplomasia katika miji mikuu yao,'' iliongeza taarifa hiyo.

Nchi hizo mbili pia ziliapa ''kupanua uhusiano wa miundombinu'' ili kukuza biashara na uwekezaji.

Mzozo kati ya Ethiopia na Somalia ulianza Januari 2024, wakati Ethiopia ilitia saini mkataba na eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland kutumia bandari ya Bahari Nyekundu ya Berbera.

Tangu wakati huo, Uturuki imefanya kazi ili kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo mawili.

Azimio la Ankara lilifikiwa mwezi Disemba mwaka jana wakati wa mazungumzo yaliyoandaliwa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, na viongozi wa Somalia na Ethiopia walihudhuria.

TRT Afrika