Wajumbe kutoka Ethiopia, Misri na Sudan wamekamilisha awamu ya kwanza ya mazungumzo ya pande tatu kuhusu ujazaji na uendeshaji wa kila mwaka wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD).
Mkutano huo ulifanyika Cairo mji mkuu wa Misri.
Bwawa la GERD linajengwa na Ethiopia na linatarajiwa kuwa na ukubwa wa kuzalisha Megawati 6000 ya umeme.
Hata hivyo kumekuwa na mvutano kati ya Ethiopia , Sudan na Misri huku nchi hizi mbili zikidai zinataka kushirikishwa katika ratiba ya Ethiopia ya kujaza bwawa hili.
Zimedai kuwa ikijazwa hadi juu basi huenda ikapunguza maji ambayo yanatiririka kuingia nchi zao kutoka mto Nile.
Ujazaji maji kwa njia ambayo haithuru nchi zingine ndiyo msingi wa mazungumzo haya kati ya Ethiopia , Misri na Sudan.
"Tumejadili vifungu kadhaa na tunaendelea na mazungumzo ili kufikia makubaliano kamili," balozi wa Ethiopia Marekani Seleshi Bekele amesema katika mtandao wake wa X.
Balozi Seleshi Bekele ni mkuu wa mazungumzo upande wa Ethiopia.
"Ethiopia inajadiliana kwa nia njema, ambapo manufaa makubwa ya GERD kwa Waethiopia yanapatikana, ushirikiano kati ya mataifa yetu ya pwani unaimarishwa kwa kuzingatia kanuni zinazohakikisha matumizi ya haki na ya kuridhisha ya maji ya Mto Nile katika siku zijazo," ameongezea.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia inasema mazungumzo hayo " yalihusisha mawazo ya makubaliano."
"Mazungumzo hayo yalianza tena kufuatia mashauriano baina ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na Rais Abdel Fattah Al-Sisi wa Misri mnamo Julai 13, 2023," wizara ya mambo ya nje imesema.
Misri , Ethiopia na Sudan zimekubaliana kuwa mkutano ujao utafanyika mwezi September 2023, jijini Addis Ababa.
Kwanini bwawa la GERD linazua mvutano?
Mradi wa kujenga bwawa kubwa la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) lenye thamani ya dola bilioni 4.2 ilianza mwaka 2011.
Ethiopia inaliangalia kama chanzo cha umeme katika nchi yake ambapo zaidi ya asili mia 60 ya watu hawana umeme. Nchi jirani kama Kenya pia zinangoja kununua umeme kutoka kwa bwawa.
limejengwa katika mto Nile na inakadiriwa kuwa ili kufikia kilele cha operesheni yake , itahitaji tani bilioni 72 ya maji kujazwa kwenye bwawa hilo.
Misri na Ethiopia, majirani wawili wakubwa wa Sudan, wamekuwa katika mzozo kwa miaka ya hivi karibuni kuhusu ujenzi wa bwawa kubwa Grand Ethiopian Renaissance (GERD) la kuzalisha umeme kwenye Blue Nile, karibu na mpaka na Sudan.
Ethiopia tayari imeanza kujaza bwawa hili, jambo ambalo Misri na Sudan zimeendelea kupinga zikitaka kuhusishwa kwani pia nchi hizo zinategemea maji ya mto Nile.
Misri inaiona GERD kama tishio lililopo kwa sehemu yake ya maji kutoka Nile na inataka Addis Ababa kufikia makubaliano ya lazima juu ya kujaza na uendeshaji wa bwawa hilo.
Ethiopia inaona bwawa hilo kama chanzo muhimu kwa mchakato wake wa maendeleo na inakanusha madhara yoyote kwa sehemu ya maji ya Misri na Sudan, nchi mbili za chini ya mto.