Ethiopia imekuwa ikishinikiza kuvutia uwekezaji wa kigeni. / Picha: AFP

Ethiopia inalenga kupitisha sheria ya kuruhusu wageni kumiliki mali kama nyumba na ardhi kama sehemu ya mpango mpana wa nchi hiyo wa kufungua uchumi na kuvutia wawekezaji, Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema kwenye TV ya taifa Jumamosi jioni.

Hivi sasa wageni wamezuiwa kumiliki nyumba nchini Ethiopia, ama majengo ya makazi au ya kibiashara, jambo ambalo linaonekana kuwa kikwazo kwa juhudi zinazoendelea za kuvutia uwekezaji wa kigeni katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Televisheni ya Taifa ilisema Abiy aliuambia mkutano wa walipa kodi wakubwa katika mji mkuu Addis Ababa kwamba serikali yake inakamilisha sheria mpya ya kuwaruhusu wageni kumiliki mali isiyohamishika ingawa hakusema ni lini sheria hiyo itawasilishwa bungeni.

"Tutaanzisha sheria ambayo itaruhusu wageni kumiliki mali," alisema, akiongeza kuwa serikali pia inakusudia kurekebisha sheria zilizopo ili kufungua sekta ya rejareja nchini, ambayo kwa sasa inahusu Waethiopia pekee.

'Kuwa tayari'

"Ilikuwa (uchumi) imefungwa, lakini sasa tutaifungua kidogo. Kwa hiyo tunataka nanyi muwe tayari," alisema.

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya Abiy imekuwa ikifungua sehemu za uchumi unaodhibitiwa vikali kama vile mawasiliano ya simu na benki kwa uwekezaji wa kigeni, kama sehemu ya mpango wa kuongeza mapato ya mitaji ya kigeni ili kukuza ukuaji na kuunda ajira kwa nchi ya zaidi ya watu milioni 100.

TRT Afrika