Makasisi wa Kanisa la Othodoksi wakiimba walipokuwa wakifanya misa ya kitamaduni kwa Mwaka Mpya wy Ethiopia mjini Addis Ababa./ Picha : Reuters 

Na Dayo Yussuf

Melkam Enkutatash !

Hii ni salamu ya heri ya mwaka mpya, nchini Ethiopia. Maana Septemba 11, nchi hiyo inasherehekea mwaka mpya wa 2017.

Lakini kwanini wanasherehekea mwaka mpya kati kati ya mwaka unauliza?

Ili kuelewa hili, ni muhimu kurejelea historia ya Ethiopia kwa karne na karne zilizopita.

Ethiopia imejiimarisha kama taifa la kipekee sio Afrika tu bali duniani kote.

Taifa hili linatajika kama mojawapo ya nchi za kale, ambazo utalikuta limetajwa katika bibilia, Korani na maandishi mengine ya kale.

Mfano katika kitabu cha Kiislamu Quran, nchi hii imetajwa katika historia ya mwanzo mwanzo wa Uislamu ambapo Mtume Muhammad (amani imfikie) aliposhambuliwa na Waarabu wa Makka, mji alikozaliwa, aliwaamrisha wafuasi wake waliokuwa wachache mno wakati huo, kukimbilia kutafuta hifadhi nchini Ethiopia, wakati huo maarufu kama Abbisynia.

Abbisynia ilikuwa inatawaliwa na mfalme Najash wakati huo, mflame Mkristu aloyesifiwa kwa uadilifu wake na haki.

Lakini hata nyyuma kabla ya hapo, Ethiopia inatajwa katika Bibilia na vitabu vingine vya historia kwa uhusiano na mfalme Solomon wa Israeli.

Malkia wa Uhabeshi, aliyejulikana kama Queen of Sheba, alipata mualiko kutoka kwa mfalme Solomon, na alipokwenda kumzuru, mwanzoni alitaka kubishana naye juu ya imani na didni yake. Lakini badala yake alirudi akiwa amekumbatia dini ya mflame Solomon na kuieneza katika ardhi yake.

Enkutatash ni neno linalotokana na ziara hii, ambapo Queen of Sheba alimpelekea mflame Solomon zaidi ya Tani nne za dhahabu kama zawadi, na aliporudi nyumbani, wananchi wake walimpokea kwa zawadi za dhahabu na mali zingine, na ndio maana ya Enkutatash.

Tukirudi kwa suala la turathi ya taifa hilo kongwe zaidi barani Afrika, Ethiopia haijawahi kutawaliwa na mgeni, au kuwa chini ya ukoloni wa aina yoyote.

Hii ina maana iliweza kuhifadhi historia yake, lugha, dini, utamaduni na turathi zake kama ilivyokuwa tangu jadi. Tia mstari 'dini' kwa kuwa tukirejelea itakufahamisha zaidi namna dini ya Waethiopia inashawishi Kalenda yao.

Maua ya manjano - Adey Abeba

Kimsingi Ethiopia inaingia leo Septemba 11 mwaka wao wa 2017. Hii inaiweka nyuma ya dunia kwa takriban miaka 7.

''Wengi wetu tunapenda kumbukumbu zetu nzuri za utoto kusherehekea mabadiliko ya mwaka na familia na jamaa wa karibu,'' anasema Kidus, Muethiopia anayeishi London.

''Kwa kweli ni maalum. Inathaminiwa sana na Waethiopia walioko ughaibuni ambao malezi yao yalikuwa Ethiopia,'' Kidus anaambia TRT Afrika. ''Tunajikuta tuko mbali na nchi yetu ya mama, inatukumbusha mengi,'' anasema.

Tarehe hii huambatanishwa na kumalizika kwa msimu wa mvua na kuanza kwa msimu wa kiangazi. Maeneo mengi nchini Ethiopia yanakuwa yametanda rangi ya manjano kutokana na maua yanayotanua.

Kutanua Maua ya Adey Abeba huashiria mwanzo mpya na huambatana na mwaka mpya /Picha: Reuters 

Waethiopia wanapambia ua hili kusherehekea mazao, msimu mpya na mwanzo mpya.

''Kama watoto, tungejipamba kwa maua ya Adey Abeba na kwenda kutoa salamu za Mwaka Mpya huku tukizunguka na kuwauzia majirani zetu maua hayo,'' anakumbuka Kidus.

Sasa hii yote inahusiana vipi na kalenda ya Ethiopia ?

Ge-ez

Kalenda yake inajulikana kama Ge’ez ama Ethiopic Calendar.

Wengine wote duniani wanatumia kalenda ijulikanayo kama Gregorian Calendar ambayo ilianzsihwa mnamo Oktoba 1582 na Papa wa Katoloki Gregory wa 13.

Kalenda hii ilisambazwa na viongozi wa katoliki na wakoloni walipo tawala Afrika na maeneo mengine.

Lakini Kama tujuavyo Ethiopia haikuwa chini ya ukoloni wowote kwa hiyo haina shinikizo lolote kwa mifumo yake. Kwa hiyo nchi iyo inafuata Kalenda yake ya tangu jadi kulingana na hesabu zake.

Kalenda ya Ethiopia ina miezi kumi na mbili zilizo na siku thelathini kamili kila moja, lakini pia wana mwezi mmoja wa ziada wa kumi na tatu ambao una siku tano au siku 6 katika mwaka wa leap year.

Lakini tofauti ya miaka 7 kati ya kalenda ya Ethiopia na wengine duniani inatokana na tofauti ya hesabu ya tarehe ya kuzaliwa wa Yesu Kristo kwa mujibu wa historia yao.

Kwa mujibu wa Kalenda ya Ethiopia, Yesu Kristu alizaliwa mwaka wa 7BC huku Kalenda ya Gregorian tunayotumia sisi inasema Yesu Kristu alizaliwa 1 AD, ambayo ni karne mbili na miaka 24 zilizopita, na hivyo kusababisha tofauti ya miaka saba iliyoachana na Waethiopia.

Kalenda ya Gregoria hata hivyo imewahi kutiliwa dosari mara kadhaa huku Papa mtakatifu Benedikt wa kumi na sita aliwahi kukosoa kuwa Kalenda ya Kikristu imehasabiwa kimakosa na kuwa Yesu Kristu alizaliwa mapema kuliko inavyodaiwa.

Sio hilo tu, Kalenda ya Ethiopia pia inatambua January 7 kama tarehe ya kuzaliwa kwa Yesu Kristu kwa hiyo hata sherehe yao ya Ksrismasi ni tofauti na wengine.

Waumini wa kanisa la Orthodox ya asili wengi wanafuata tarehe hizi za Ethiopia kuhusu kuzaliwa kwa Yesu Kristu.

Kwa hiyo tofauti na namna watu wamezoea kusema, Ethiopia haipo nyuma ya dunia nzima kwa miaka saba, la! Wako pamoja nasi, ila namna wanahesabu tarehe zao ndio tofauti. Na hii imechangia pakubwa kuhifadhi turathi ya nchi hiyo kama ilivyokuwa tangu jadi.

Katika maadhimisho ya Enkutatash, jamaa marafiki na majirani hukusanyika pamoja kucheza densi za iskita,/ Picha : Reuters 

Sherehe, densi na mlo!

Maadhimisho ya siku hii kubwa yanakuja kwa njia tofauti kila sehemu ya nchi.

''Ndugu zetu wangetutembelea wakati wa likizo na kuleta binamu zetu na tungecheza tu pamoja. Likizo zilileta watu pamoja,'' anasema Kidus.

Hii ina maana mlo wa kila aina. Injera, mkate wa asili wa Ethiopi unaotengenezwa kwa unga wa Teff uliochachishwa, huandaliwa kwa mchuzi wa rigirigi wa kuku, mayai na vioungo vingine, mchuzi wa shiro, nyama ya kondoo na mboga mboga zingine.

Pia chakula huteremshwa kwa kinywaji cha asili, Tej. Huu ni mvinyo unaotokana na asali, maarufu sana Ethiopia na Eritrea. Una kileo cha asili mia 70 kwa hiyo ni kinywaji cha watu wazima.

Kisha jamaa marafiki na majirani hukusanyika pamoja kucheza densi za iskita, kunywa kahawa na kufurahia siku. wakati mwingine sherehe hizi zinaweza kwenda zaidi ya wiki moja.

Mfumko wa bei, majanga ya ukame na mafuriko na vurugu za kisiasa zimekuwa na athari kubwa kwa hali ya kiuchumi ya Waethiopia wengi. / Picha : Reuters 

Changa moto za kiuchumi

''Ukitazama sherehe zinavyofanyika sasa na ilivyokuwa tulivyokuwa wadogo, mambo yamebadilika,'' anasema Kidus. ''Uchumi umekuwa mgumu. sasa watu hawawezi kumudu sherehe za muda mrefu, au za gharama kubwa,'' anaongeza.

Mfumko wa bei, majanga ya ukame na mafuriko na vurugu za kisiasa zimekuwa na athari kubwa kwa hali ya kiuchumi ya Waethiopia wengi.

Bidhaa zimepanda bei kwa kiasi kikubwa huku wengi wakilazimika kukimbia makwao kutokana na ukosefu wa usalama. Hii imeathiri namna Waethiopia wengi wanasherehekea siku hii ambayo kimsingi ilitakiwa kuwa ya furaha.

Wale waliolazimika kukimbia nchi wanasema wanategemea kumbukumbu za utotoni kuweza kutabasamu kwa siku hii.

''Tunajikuta tuko mbali na nchi yetu ya mama. Kumbukumbu hizi ndizo tunashikilia kwa nguvu kwani ziko karibu sana na moyo,'' anasema Kidus, akiwa London.

Basi ukikutana na Mu Ethiopia wiki hii, mwambie Melkam Enkutatash!

TRT Afrika