Mawaziri wa kisekta kutoka EAC wamezitaka nchi wanachama kutumia mifumo ya kidijitali katika kuondoa Vikwazo vya Kibiashara Visivyo vya Kiforodha, maarufu kama NTBs.
Mawaziri hao, wanaowakilisha sekta za Biashara, Viwanda, Uchumi na Uwekezaji (SCTIFI), waliokutana jijini Arusha, Tanzania kwa ajili ya mkutano wao wa 43, pia wamezitaka nchi wanachama kuanza uhamasishaji wa teknolojia hiyo, ifikapo Aprili 30, 2024.
Teknolojia hiyo ya simu, iliyobuniwa na Trademark Africa inalenga kutoa taarifa na kufuatilia na kuondoa vikwazo hivyo.
Programu hiyo inawawezesha watumiaji kutoa taarifa za malalamiko ya uwepo wa vikwazo hivi, kwa kutumia lugha za Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa.
Sekretariati ya EAC kwa kushirikiana na na Trademark Africa walizindua programu hiyo katika maonesho ya wajasiriamali wa EAC, uliofanyika Disemba 8, mjini Bujumbura, Burundi.
Kwa muda mrefu, uwepo wa vikwazo hivyo vya kibiashara umesababisha nchi wanachama kushindwa kufanya biashara kati yao.
Hata hivyo, mawaziri hao wa kisekta walijulishwa kuwa vikwazo viwili kati ya tisa vimekwishaondolewa, kati ya mwezi Julai na Novemba, 2023. Jumla ya vikwazo 269 vimeondolewa toka mwaka 2007.
Mawaziri hao, pia walizitaka nchi za Tanzania na Kenya kufanya uhakiki wa pamoja wa vifaa vya pikipiki zilizosafirishwa kutoka Kenya kwenda Tanzania, na kuwasilisha ripoti ya mchakato huo kwenye mkutano wa 45 wa mawaziri hao wa kisekta.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa EAC, Peter Mathuki,amesema kumekuwa na mwenendo wa kukua kwa biashara ya ndani baina ya nchi wanachama
“Katika mwaka wa fedha wa 2021 / 2022, thamani ya biashara ya ndani ilifikia dola bilioni 8.7, ambayo ilikuwa hadi dola bilioni 9.4 katika mwaka wa fedha wa 2022/2023. Hii inaonesha uimara wa mazingira ya kufanya biashara katika ukanda wetu,” alisema Mathuki.