Ramadhan Kibuga
TRT Afrika, Bujumbura, Burundi
Huku kampeni za uchaguzi mkuu zikiendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiwa imesalia chini ya mwezi moja kabla ya Uchaguzi wa Urais kufanyika, waasi wa M23 wameendelea kusonga mbele katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.
Kwenye taarifa yake ya Alhamisi, kikundi hicho kimetangaza kuuteka mji wa Mweso katika Kivu ya Kaskazini.
Mji huo unapatikana umbali wa kilomita 100 na mji mkuu wa mkoa huo, Goma.
Kulingana na asasi za kiraia za eneo hilo, kijiji cha Mweso kilikuwa hakina watu tangu Alhamisi tarehe 23 Novemba.
Maelfu ya wakazi wake na wakimbizi wa ndani walitoroka makazi yao na kukimbia baada ya mashambulizi wa waasi wa M23 kufuatia siku kadhaa za makabiliano na makundi ya wanamgambo maarufu 'Wazalendo' waatiifu wa serikali ya Kinshassa.
Udhibiti wa mji wa Mweso waashiria hatua mpya ya muendelezo wa kuyateka maeneo mapya ya Mashariki mwa Congo.
Lakini pia inaruhusu waasi hao kuvunja moja ya barabara zinazoelekea mji wa Goma, Kaskazini mwa mkoa huo.
Kikundi cha waasi wa M23 wameendesha operesheni ya kudhibiti maeneo ya Kusini.
Na sasa waasi hao wa M23 wanapatikana umbali wa kilomita 20 na mji wa Saké kwenye mwambao wa Ziwa Kivu.
Kwa mujibu wa wadadisi, utekaji wa miji hiyo miwili utaruhusu waasi wa M23 kusimamia na kudhibiti biashara zinazoelekea mji wa Goma.
Na kuna uwezekano mkubwa wa uzalishaji wa mazao kuathirika katika mji huo mkuu wa Kivu Kaskazini, hasa upande wa eneo la Masisi.
Haya yanajiri wakati kampeni ya uchaguzi mkuu wa Disemba 20 inaendelea nchini DRC.
Na kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa kampeni hizi mapema tarehe 20 Novemba, mji wa Goma hafla hii ilifikia watu wa Goma.
Moïse Katumbi Chapwe alikusanya maelfu ya wafuasi wake katika uwanja wa Afya mjini Goma baada ya kutembea kwa mguu kutoka uwanja wa ndege wa Goma.
Gavana huyo wa zamani wa Katanga ameahidi iwapo atachaguliwa kuimarisha amani Mashariki mwa Congo pamoja na ujenzi mpya wa mikoa ya Kivu ya Kaskazini na Ituri kwa kutenga zaidi ya dola bilioni tano.
Huku mashambulizi haya yakianza msimu wa mvua umeanza na maelfu walikimbialia makambini wanateseka zaidi.
"Unapojaribu kulisha zaidi ya watu milioni tatu na laki sita walio makambini, na wanaishi kwa maeneo kama haya, hali hii inafanya maisha yako kuwa magumu zaidi licha ya wao kuwa na uvumilivu," anasema Shelley Thakral, msemaji wa Shirika la Chakula Duniani nchini DRC.
Wakati huo huo, viongozi wa mataifa ya Jumuia ya Afrika Mashariki, wanakutana jijini Arusha kaskazini mwa Tanzania katika mkutano wa kawaida. Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa na viongozi hao, ni pamoja na usalama wa DRC.