Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC imeanza shughuli ya kupeleka majeshi yake katika eneo la Mashariki mwa DRC.   

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC imeanza shughuli ya kupeleka majeshi yake katika eneo la Mashariki mwa DRC. Ahadi hiyo ilitangazwa mapema tarehe 8 mwezi Mei wakati wa mkutano wa kilele wa marais uliofanyika nchini Namibia. Miezi saba baadae, wanajeshi wa Afrika ya Kusini waliwasili mjini Goma. Hata hivyo bado kuna maswali mengi kuhusu utaratibu huo wa kupeleka vikosi hivyo vya SADC.

Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC imeanza shughuli ya kupeleka majeshi yake katika eneo la Mashariki mwa DRC.

Swali la kwanza ni kuhusu idadi ya vikosi hivyo.Wanajeshi wa kwanza walitua tarehe 27 katika uwanja wa Goma, lakini msemaji wa Jeshi la Congo 'FARDC' katika Ukanda huo hakutaja idadi ya vikosi ambavyo tayari vimewasili. Baadhi ya duru zinasema kwa hatua ya kwanza wanajeshi hao wanakadiriwa 200. Na hivi karibuni wanajeshi wengine kutoka vikosi vya Tanzania,Malawi watajiunga na vikosi hivyo kutoka Afrika ya Kusini. Lakini tarehe ya kuwasili bado kufahamika.

Kwa mujibu wa taarifa ya SADC ya mapema tarehe 14 mwezi huu, vikosi hivyo vitakuwa na muhula wa kipindi cha miezi 12 na watapeleka brigedia ya wanajeshi 7000 ikiwa ni pamoja pia na usaidizi wa Jeshi la anga, vikosi vya wanamaji pamoja na zana nzito nzito.

Kimsingi vikosi hivyo vya SADC vinakuja ''kuunga mkono nchi ya DRC kumaliza makundi ya waasi katika eneo la Mashariki mwa nchi'' kulingana na taarifa hiyo ya SADC. Lakini taarifa hiyo haiweki wazi ni vikundi gani SADC watapambana navyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa Waziri wa mambo ya kigeni wa DRC Christophe Lutundula, vikosi hivyo watakuwa pakubwa na shughuli ya kupambana na waasi wa M23 ambao wanadhibiti sehemu ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini.

Wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki walikuwa na jukumu hilo hilo. Lakini walilazimishwa na Serikali ya Kinshassa kuondoka Mashariki mwa nchi hiyo kwa madai kwamba wameshindwa kukabiliana vilivyo na waasi kwenye maeneo hayo. Kikosi cha mwisho cha Kenya kiliondoka tarehe 21 Disemba.

Burundi ni nchi pekee ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki imesalia na vikosi katika Congo, lakini ni katika mpango wa ushirikiano wa kiusalama na ulinzi kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema vikosi vyake vimekwenda nchini DRC kukabiliana na waasi wa Burundi wa RED Tabara ambao wanaripotiwa Mashariki mwa Congo.

Harakati hizo za kijeshi za SADC zinafanyika wakati shughuli ya uhesabiaji wa kura ikiendelea kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe 20 Disemba. Rais aliye madarakani Felix Tshisekedi anaongoza kwa wingi mkubwa wa kura katika kinying'anyiro cha Urais wakati Upinzani ukidai kwamba uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu mkubwa pamoja na dosari nyingi.

TRT Afrika