Idara ya mashtaka ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, DRC, imetoa taarifa kuwa mshukiwa wa kwanza alikamatwa akihusishwa na mauaji ya mpinzani Cherubin Okende.
"Tunamfuatilia mhalifu mmoja kwa sasa, tumemtia nguvuni, ni mtuhumiwa wa kwanza anayehojiwa na mahakama kuu", amesema Firmin Mvonde Mambum mwendesha mashtaka mkuu.
''Uchunguzi umeanza, polisi wa kisayansi wameitwa kwani kifo hicho kilitokana na risasi, risasi iliyopatikana karibu na marehemu.'' aliongeza Bw Firmin.
Mwili wa mbunge huyo wa Kongo Chérubin Okende, ambaye alikuwa pia msemaji wa chama cha siasa cha Ensemble pour la République, ulipatikana Alhamisi, Julai 13 kwenye gari lake.
Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha mwili wa Cherubin Okende, ambaye aliwahi pia kuwa Waziri wa Uchukuzi, ukiwa umepigwa risasi ndani ya gari lake.
Hali ya wasiwasi ilitanda huku baadhi ya watu wakianza maandamano katika mji mkuu baada ya kuthibitishwa habari za kifo chake.