Bintou Keita, kiongozi wa Umoja wa mataifa DRC akiwa Goma / Photo: Reuters

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kikosi cha Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, MONUSCO, Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini, Bi Bintou Keita ameomba waasi wasitishe vurugu, waweke chini silaha zao na warudi katika nchi zao za asili.

"Monsuco imepokea taarifa za mauaji ya raia mnamo Aprili 6, lakini mauaji hayo yanayohusishwa na wanamgambo wa Allied Democratic Forces (ADF) yaliyotokea Aprili 2 na 3 kwenye mipaka kati ya eneo la Mambasa na Irumu," alisema Bi Keita.

Kiongozi wa asasi za kiraia katika kijiji jirani cha Kilya, Bw Moise Kalwana aliieleza TRT Afrika kwamba alikutana na mabaki ya binadamu na mifupa kama vile kaburi la watu wengi katika mashamba ya watu ambao inasemekana waliuwawa na waasi.

"Tumeshatoa taarifa kwa mamlaka husika kusema wawazike watu hata kwenye kaburi la pamoja. Kwa kweli, inatisha hata kuona mifupa ya binadamu." alieleza Kalwana.

ADF ni kina nani?

ADF ni Allied Democratic Forces ambao ni kundi la waasi kutoka Uganda wenye makao yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Uganda inasema kwamba ADF ni kundi la kigaidi. Walianzia Uganda Magharibi wakahamia DRC.

Inaaminika kuwa ADF walihusika na tukio la shambulizi la bomu, mwezi wa Januari, katika mkoa wa Kivu Kaskazini nchini DRC. Mashambulizi yalilenga kanisa na kuwaua watu 17.

TRT Afrika