Rais Felix Tshisekedi alitangaza siku ya kitaifa ya maombolezo Jumatatu kwa heshima ya wahathiriwa, na serikali kuu inatuma timu ya kudhibiti shida huko Kivu Kusini kusaidia serikali ya mkoa.
Takriban miili 203 imeopolewa kutoka Kalehe, eneo lililoathiriwa zaidi na mafuriko katika jimbo la Kivu Kusini, mashariki mwa DRC.
"Hapa Bushushu, miili 203 tayari imeondolewa kwenye vifusi," Thomas Bakenga, msimamizi wa eneo la Kalehe, ambako vijiji vilivyoathiriwa vinapatikana, alisema Jumamosi.
Haikuwezekana kutathmini kiwango cha majeruhi wote wa kibinadamu na uharibifu wa nyenzo, aliambia vyombo vya habari vya ndani.
Idadi ya muda, iliyotangazwa Ijumaa mwishoni mwa siku na gavana wa jimbo hilo, iliripoti angalau 176 waliokufa.
Mvua kubwa iliyonyesha Alhamisi katika eneo la Kalehe mkoani Kivu Kusini ilisababisha mito kufurika na maporomoko ya ardhi kukumba vijiji vya Bushushu na Nyamukubi.
Kwa jumla, vijiji kadhaa viliathirika na maji, nyumba nyingi zilisombwa na maji na mashamba kuharibiwa, wakati mito katika mkoa huo ilipasua kingo zake kutokana na mvua kubwa.
Daktari wa Kongo na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Denis Mukwege, ambaye kliniki yake iko Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini, alisema siku ya Jumamosi alituma timu ya madaktari wa upasuaji, madaktari wa ganzi na mafundi katika eneo hilo "kuwapa watu msaada wa dharura wa matibabu. ".
"Hatuna kingine hapa"
Michake Ntamana, mfanyakazi wa uokoaji anayesaidia kuwasaka na kuwazika maiti, alisema wanakijiji wanajaribu kutambua na kukusanya miili ya ndugu waliopatikana hadi sasa.
Alisema baadhi ya miili iliyosombwa na maji kutoka vijiji vilivyo juu ya vilima ilizikwa ikiwa imefungwa kwa majani ya miti. "Inasikitisha sana kwa sababu hatuna kitu kingine chochote hapa," alisema.
Maafa hayo yametokea siku mbili baada ya mafuriko kuua takriban watu 131 na kuharibu maelfu ya nyumba katika nchi jirani ya Rwanda.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumamosi alitoa salamu za rambirambi kwa wahanga wa "mafuriko makubwa" nchini Rwanda na DRC.
"Hiki ni kielelezo kingine cha kuharakisha mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake mbaya kwa nchi ambazo hazijafanya lolote kuchangia ongezeko la joto duniani," alisema wakati wa ziara yake nchini Burundi.
Wataalamu wanasema matukio ya hali ya hewa kali yanazidi kuwa ya mara kwa mara na makali kutokana na mzozo wa hali ya hewa.