Na Lulu Sanga
Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano Mashariki, Mhe. Dkt Stergomena Tax inasema kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na taarifa sahihi za watu ambao wamekuwa wakichangia na kukuza uchumi wa nchi hiyo.
“Mfumo huu utaisaidia Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora wake, utawezesha Diaspora kufahamu na kupata taarifa zinazo husu masuala mbalimbali ya Diaspora ambapo tunashuhudia ushiriki wa Diaspora katika kujenga uchumi wa Taifa letu ukiendelea kukua siku hadi siku,” alisema Dkt. Tax.
Hata hivyo Tanzania imewataka Diaspora wake wautumie Mfumo huo ili kuiwezesha Serikali kupata kanzidata itakayoiwezesha kupanga mipango mbalimbali na kuwawezesha Diaspora kupata fursa zilizopo nchini.
TRT Afrika imezungumza na Khamis Iddi Khamis diaspora wa Tanzania nchini Uturuki anasema hii ni hatua nzuri kufanywa na serikali kwani bado wanamajukumu mengi nyumbani.
"Sisi sote ambao tuko nje ya nchi kikazi au kimasomo au hata kwa sababu nyingine tuna mchango mkubwa sana katika maendeleo ya jamii yetu. Ukizingatia si ukoo mzima wa diaspora fulani wote uko nje ya nchi. Wengi tuna majukumu nyumbani na tunayatekeleza japo tukiwa mbali", anamaliza Khamis
Vipi kuhusu mapato yatokanayo na Diaspora nchini Tanzania
Tanzania imeweka wazi kuwa mchango wa Diaspora katika uchumi unaonekana kupitia takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Tanzania ambapo katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 Diaspora walituma Tanzania Dola za Marekani Milioni 569.3.
Hata hivyo mwezi Januari hadi Desemba 2022 diaspora hao walivunja rekodi yao kwa kutuma nyumbani Tanzania kupitia vyanzo rasmi Dola za kimarekani Bilioni 1.1 ambazo ni sawa na Shilingi Trilioni 2.6 za Tanzania.
Pia imefafanuliwa kuwa Diaspora hao kwa mwaka 2021 walinunua nyumba na viwanja Tanzania kwa thamani ya Shilingi Bilioni 2.3 na mwaka 2022 walitumia Shilingi Bilioni 4.4 kununua Nyumba na Viwanja nchini.
Tofauti na hilo mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja (UTT-AMIS), unaonesha kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2022 Diaspora waliwekeza Shilingi Bilioni 2.5 katika mifuko mbalimbali ya UTT- AMIS.
Tanzania imeweka wazi kuwa mchango wa watanzania au watu wenye asili ya Tanzania ughaibuni ni mkubwa katika kuimarisha uchumi wa nchi hiyo na watahakikisha kanzidata inayoundwa itawafaidisha diaspora hao kwa fursa zinazopatikana nchini humo.