Prep imepata umaarufu kama dawa inayosaidia kuzuia maambukizi hasa kwa wanaokabiliwa na tisho kutokana na mtindo wa maisha au kazi wanazofanya/ Picha: Getty

Na Dayo Yussuf

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Kila mwaka ifikapo siku hii, watu huangazia Ugonjwa wa UKIMWI, virusi vyake, maambukizi, tiba, utafiti, yaani kila kitu kinachohusiana na ugonjwa huo.

Takriban miaka 30 au 40 iliyopita, kupata maambukizi ya HIV ilichukuliwa kama hukumu ya kifo. Hakukuwa na matumaini kabisa, na hakukuwa na utafiti wa kutosha. Tiba hakuna na njia za kujizuia ndio zilikuwa ngumu zaidi hasa kwa watu wanaotishiwa kila siku kutokana na shughuli zao au mtindo wa maisha.

Mbali na utafiti wa dawa za kutibu au kupunguza makali ya virusi hivyo, kumekuwa na hatua kubwa katika kutafuta kinga ya virusi hivyo.

''Mimi nilikwenda kutafuta Prep, lakini mwanzo wakaniambia sitakiwi kutumia.''

Jeffrey Walimbwa anazungumzia dawa ambayo imeanza kupata umaarufu nchini Kenya iitwayo Prep, yaani Pre Exposure Prophylaxis.

Hii ni dawa inayosaidia kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV kwa watu ambao hawajaambukizwa virusi hivyo, lakini wanakabiliwa na tisho la maambukizi.

Jeffrey anasema kuwa yeye alikuwa anajihusika mapenzi bila kinga. Hivyo, aliposikia kuhusu Prep alipendelea kuanza kuitumia.

''Hawakuwa na maelezo ya kutosha juu ya dawa hizo. Kwa hiyo hawakunipa," Jeffrey anaambia TRT Afrika.

Aina za Prep

Licha ya umuhimu wa dawa za Prep, katika vita dhidi ya maambukizi ya HIV, ukosefu wa taarifa za kutosha unaonekana kuzuia matumizi ya dawa hizi.

Nchi nyingi zimeidhinisha utumiaji wa vidonge vya Prep huku ile ya sindano ikiendelea kufanyiwa utafiti zaidi / Picha : Getty 

Prep inapatikana katika aina mbili: Katika mfumo wa vidonge na sindano. Vidonge vya Prep, (Truvada na Descovy) vinakuja kwa rangi ya buluu, na utumiaji wake umeidhinishwa na serikali nyingi zikiwemo za Afrika, na pia nchi nyingi zinasambaza dawa hizi kupitia vituo vya umma vya afya au mashirika yasiyo ya kiserikali.

Aina ya pili, ni kupitia sindano, ambayo inaitwa Appretude. Hata hivyo, hii bado inafanyiwa utafiti zaidi na utumiaji wake haujaidhinishwa na mataifa mengi ya Afrika.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa CDC, Prep inaweza kusaidia kukulinda pindi unapokuwa hujapata maambukizi ya VVU na ukawa katika mazingira yafuatayo:

  • Umehusika katika tendo la ndoa katika muda wa miezi 6 iliyopita bila kutumia kinga.

  • Kuwa na mpenzi aliye na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (haswa ikiwa kiwango cha virusi hakijulikani au kinaweza kutambulika).

  • Una mpenzi ambaye hajatumia kinga mara kwa mara.

  • Wewe au mpenzi wako amepatikana na ugonjwa wa zinaa katika kipindi cha miezi 6 iliyopita.

  • Unatumia dawa za kulevya na unatumia sindano

Wataalamu wanasema kuwa Prep inaweza kutumiwa hata na mama mja mzito, ila ni muhimu kwanza kupata ushauri wa daktari, maana inaweza kuepusha maambukizi kwa mama, mtoto aliye tumboni au hata mtoto wakati wa kunyonya.

Utumiaji wa Prep umeongezeka mara dufu hasa kwa watu wanaojikuta katika hatari ya maambukizi ya mara kwa mara. Lakini kila mtu anayetaka kujiepusha na maambukizi anaweza kutumia.

''Kumekuwa na unyanyapaa dhidi ya wanaotumia Prep. Wengi wanaona kuwa ni ya watu walio na wapenzi wengi, au wanaofanya biashara ya ngono,'' anaelezea Jeffrey. ''Hii inafanya watu wengi kuogopa kunyanyapaliwa na imeathiri sana matumizi yake,'' anaongezea.

Dawa za Prep zinasaidia kuepuka maambukizi kwa asilimia 99, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani/ Picha: Getty 

Hakuna madhara ya kutumia Prep

''Kuna mtu anasema anatumia Prep, lakini kwa siri kwa sababu mpenzi wake anaamini ukitumia inamaanisha tayari una maambukizi ya HIV,'' anasema Jeffrey.

Kituo cha kudhibiti magonjwa CDC kinasema kuwa Prep haina madhara makubwa yanayojulikana, ila kuna ripoti chache za watu kuharisha, kuumwa na kichwa, maumivu ya mwili, kichefuchefu au kuumwa na tumbo. Ila wale wanaopata madhara mengi zaidi au dalili hizi kukaa muda mrefu, wanashauriwa kufika hospitali ili kupata usaidizi kutoka kwa wahudumu wa afya.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani WHO, bara la Afrika ndilo lina idadi kubwa zaidi ya walio na maambukizi ya virusi vya HIV, takriban milioni 25 kote barani, na pia ndilo bara lililoripoti maambukizi mapya mengi zaidi.

Huku utafiti ukiwa bado unaendelea na juhudi za kutoa hamasa na kujenga uelewa zikiendelea kote duniani juu ya tiba na namna ya kujikinga na maambukizi ni muhimu kujua angalau kuna njia rahisi ya kujiepusha iliyoidhinishwa na WHO na kupendekezwa na wataalamu wa afya.

Lakini tunaposubiri utafiti zaidi juu ya tiba, na pengine kinga bora zaidi ya maambukizi ya Ukimwi, wataalamu wanashauri kuwajibika binafsi kwa kujua hali yako, kujikinga, na iwapo umepata maambukizi, basi tumia dawa.

Kauli Mbiu: Jua Hali Yako, Jikinge, na Iwapo Umepata Maambukizi, Tumia Dawa.

TRT Afrika