Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ameandaa shughuli ya usafishaji mji utakaofanywa na vikosi vya jeshi la taifa 23-24 Januari/ Picha : TRT Afrika

Ronald Sonyo

TRT Afrika, Dodoma, Tanzania

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila ametangaza kufanyika kwa zoezi la usafi katika wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuhusisha wanajeshi zaidi ya 5000, Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Jeshi la Polisi zaidi ya 3000, kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) pamoja na vyombo vingine vya dola.

Akitangaza uamuzi huo katika ibada ya kuwekwa wakfu mwangalizi wa jimbo la Babtist la Dar es Salaam Chalamila aliwataka wakazi wa mkoa huo kutokuwa na shaka mara baada watakavyoviona vyombo vya dola vikifanya usafi.

“Na kwa mantiki hiyo sisi serikali tumeamua tarehe 23 na 24 ya mwezi huu wa kwanza tutafanya usafi katika mkoa mzima kwa kushirikiana na vyombo vya dola kwa hiyo mkiona wanajeshi wengi barabarani msiogope mjue wanafanya usafi,” alifafanua.

“Kutakuwa na wanajeshi wengi zaidi ya 5000, Polisi zaidi ya 3000, Jeshi la zimamoto,2000, watu wa usalama barabarani , JKT watu wa uhamiaji lakini katika kufanya usafi kutakuwa pia magari ya wanajeshi kwa ajili ya kukusanya taka , kwahiyo mkiwaona msiogope labda kama kuna watu amabao wamedhamiria kufanya fujo” Aliongeza Chalamila.

“Tumepata taarifa ya kuwepo kwa mlipuko wa kipindupindu mikoa kama 6 lakini Dar es salaam hatujapata kipindupindu, sasa niwaombe ndugu zangu mkawe mabalozi wazuri kwenye suala la usafi” Alisema.

Zoezi linagongana na wito wa maandamano ya Upinzani

Zoezi hilo limetangazwa kuanza Januari 23-24 mwaka huu.

RPC Albert Chalamila amewaomba wakaazi wa Daresalaam wasiwe na wasiwasi wakiona vyombo vya usalama vikifanya usafi jijini / Picha : TRT Afrika

Tangazo hilo linakuja baada ya Chama cha upinzania Nchini Tanzania –CHADEMA kuazimia kuandamana kushinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali wa uchaguzi walioyatoa hivi karibuni. Maandamano hayo yamepangwa kuanza baadaye tarehe 24 mwezi huu.

Mbali na gharama za maisha chama hicho kinasema muswada wanaopinga ni ule wa sheria ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2023, Sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi wa mwaka 2023 pamoja na muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali (No.5) wa Mwaka 2023.

Muswada mwingine pia ni ule wa sheria ya marekebisho ya sheria za vyama vya siasa wa mwaka 2023 . Ni uamuzi uliokuja siku tatu baada ya kukamilika kwa zoezi la ukusanyaji wa maoni ya wadau wa vyama vya siasa 18, taasisi za dini, wananchi na asasi za kiraia zaidi ya 400.

”Huu ni mwaka wa uchaguzi mpo tayari turudi tena kwenye uchaguzi kama wa mwaka 2019? “Alihoji Freeman Mbowe.

Ili kuendeleza demokrasia rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza juu ya maridhiano na kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara na vyama hivyo huku akitoa ahadi ya kufanywa kwa marekebisho ya sheria zinazohusu siasa na kuahidi kuukwamua mchakato wa katiba mpya.

TRT Afrika