Meya wa mji wa mashariki mwa Libya wa Derna alizuiliwa pamoja na maafisa wengine kwa tuhuma za usimamizi mbovu na uzembe wa kuporomoka kwa mabwawa yaliyofurika mji huo wiki mbili zilizopita, ofisi ya mwanasheria mkuu wa Libya ilisema Jumatatu.
Ofisi hio iliyoko katika mji mkuu wa Tripoli, imesema imetoa maagizo ya kuwazuilia maafisa wanane wa eneo hilo kutokana na kuporomoka kwa mabwawa ya maji yaloyosababishwa na dhoruba iliyosababisha mafuriko ambayo yalisomba vitongoji baharini na kuua maelfu ya watu.
Waliozuiliwa ni pamoja na meya na afisa anayesimamia rasilimali za maji, ilisema, bila kuwataja kwa majina.
Wakazi waliokuwa na hasira wamelaumu mamlaka kwa kubomoka kwa mabwawa hayo, ambayo yalikuwa yamejengwa ili kuzuia mtiririko wa maji katika mto wa msimu unaopita katikati ya jiji.
Mkataba wa 2007 wa kukarabati mabwawa haukukamilika wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza na uasi ulioungwa mkono na NATO ambao ulimwondoa Muammar Gaddafi mwaka wa 2011. Derna ilidhibitiwa hadi 2019 na wapiganaji kutoka kwa makundi yenye silaha.
Mtafaruku wa wazi
Waandamanaji walichoma nyumba ya meya Abdulmenam al-Ghaithi wiki iliyopita, na utawala mashariki mwa nchi ulisema alisimamishwa kazi na baraza zima la jiji lilifutwa kazi.
Maelfu ya watu wamethibitishwa kufariki kutokana na mafuriko na maelfu wengine bado hawajulikani walipo, huku majengo yote yakisombwa na maji hadi baharini.
Vikosi vya kimataifa vya uokoaji vinaendelea na juhudi za kuopoa miili kutoka chini ya vifusi na katika bandari ya jiji hilo, huku matumaini ya kupata manusura yakipungua.
Hatimaye juhudi za uokoaji zimefichua msuguano kati ya serikali kuu na utawala hasimu unaodhibiti mashariki mwa nchi na ambao hautambui mamlaka ya huko Tripoli.