Chama cha upinzani nchini Tanzania (CHADEMA) kimeitaka Serikali kuwasilisha Bungeni Muswada wa sheria wa kuendeleza mchakato wa katiba mpya, kwa kujumuisha muundo wa vyombo vitakavyoundwa kwa lengo la kutengenza muafaka wa kukamilisha mchakato huo.
Chama hicho pia kimesema kuwa hakikubaliani na msimamo wa Serikali wa kutoa elimu ya katiba mpya kwa kipindi cha miaka mitatu. Chadema imetaja hatua hiyo kama ni kutumia vibaya rasilimali za umma
“Vyombo vya kuendeleza mchakato wa katiba vitakavyoundwa, vipate uwakilishi wa vijana, wanafunzi ili mawazo yao yaingie katika mchakato ili tupate katiba ya watanzania wote,” amesema John Mnyika ambae ni katibu mkuu wa Chadema.
Mnyika amedai Chama cha Mapinduzi CCM kinataka kukwamisha mchakato huo wa katiba mpya kwa kisingizo cha kutaka elimu ya katiba itolewe kwa kipindi cha miaka mitatu na kusisitiza kuwa chama hicho hakikubalini na jambo hilo.
“Sasa tumekuja kwenu vijana wasomi mtapata wasaa wa kutafakari hilo na kutoa fikra bora kwa taifa, lakini sisi hatukubaliani na hatua ya serikali kutoa elimu kwa miaka mitatu,” amesema.
Mnyika aliyasema hayo kwa viongozi na wanachama wa Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati wa Chadema (Chaso) waliofika kupata mafunzo ya kujengewa uwezo wa uongozi.
Kwa upande wake, rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekiri kwamba wadau wote wanakubaliana na hitaji la marekebisho ya katiba mpya, hata hivyo, amesisitiza kwamba, marekebisho yake ni mchakato.
“Tunakubaliana na marekebisho ya katiba yetu. Tunakubali lakini jambo hili ni mchakato, na kwa bahati nzuri, katiba, si mali ya vyama vya siasa,'' amesema Rais Samia.
''Katiba ni ya watanzania, awe na chama au hana, awe na dini awe hana, mnene, mwembamba, katiba ni mali ya watanzania, kwa hiyo matengenezo yake yanahitaji tafakuri kubwa sana. Hatuwezi kuchipuka tu, lakini katiba ni kitabu, tunaweza kutengeza kitabu kizuri kutakipamba tukakiweka, wangapi wanakielewa hicho kitabu, katiba tulionayo sasa wangapi wanaielewa? Tunaanza na elimu ya watanzania,” aliongeza kusema Rais Samia.