Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amewatahadharisha raia kutoshiriki maandamano ya kila mara yanayovunja badala ya kujenga / Picha : Mtandao wa Mkoa wa Dar es Salaam .

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amekemea kwa kauli kali migomo aliyotaja kuwa inayopinga maendeleo ya nchi.

Chalamila amewaagiza wakuu wa polisi, OCD na RPC wachukue hatua kali kuwadhibiti wanaozua pingamizi na rabsha zinazotishia amani na kuhujumu maendeleo.

''Hiki mnachokifanya hapa ni uhaini. Ni siasa. Kujililisha vimachozi ni siasa,'' alisema Chalamila. '' Ninaweza nikafunga leo hii na kazi ikaendelea kesho. Naweza nikaanza kutekeleza mradi na hamtafanya chochote,'' aliongeza Chalamila.

RC huyo alikuwa akihutubia wafanyabiashara wa soko la simu2000 ambao walikuwa wamezua tetesi kutokana na madai kuwa serikali inapanga mradi wa kujenga karakana ya mabasi ya mwendo kasi katika eneo lao la biashara.

Chalamila aliyejawa na ghadhabu alibainisha wazi kuwa fununu zilizokuwa zinasambaa ni kweli.

''Sasa minong'ono mliyokuwa mnasikia kuwa kuna mradi, ni kweli,'' alisema Chalamila.

Muongozo wa utekelezaji

Hata hivyo Chalamila alitoa muongozo kuwa japo mradi utaendelea, hawawezi kufunga biashara maeneo yote. Aliwataka vyombo husika kupanga ratiba ya maeneo ya kufunga ili kuwe na ushirikiano na wafanyabiashara hao.

Chalamila alionya kuwa raia wasione kuwa ofisi yake haina mamlaka ya kutosha, ila waonyeshe heshima inayostahiki kwa mamlaka.

''Migomo migomo ya kijinga kijinga, mtu anasimama eti nimetumwa, umetumwa na nani? lazima muwe na adabu sio kuniletea mambo ya kisiasa,' aliendelea kutahadharisha Chalamila. ''Nitawavuruga!''

Chalamila alielezea kuwa mradi huo una manufaa makubwa sio kwa Dar es Salaam peke yake bali mamilioni wengine kutoka mikoani.

Hii alisema inaendana na mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuweka miundo mbinu sawa ili kubadili uchumi na taswira ya Dar es Salaam.

''Kila mmoja anapoondoka kwenye madaraka lazima awe na kitu cha kukionyesha kinachoacha legacy yake,'' alisema RC huyo.

Mnamo Julai 8, wafanya biashara hao wa simu2000 walifunga barabara na stendi wakilalamikia soko hilo kugeuzwa karakana.

TRT Afrika