Moja ya maduka ya Spaza jijini Soweto, nchini Afrika Kusini./Picha: Getty

Na Emmanuel Onyango

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Serikali ya Afrika Kusini imetangaza magonjwa yanayotokana na kula vyakula kama janga la taifa. Hatua hiyo inafuatia vifo vya watoto 23, vilivyotokea katika jiji la Johannesburg, mwezi uliopita.

Maduka maarufu, kama 'Spaza' nchini humo ndiyo yamegonga vichwa vya habari kwenye sakata hilo.

‘’Maduka haya yanakuwa wazi hata nyakati za usiku, na yana aminika sana na wakazi wa maeneo yalipo’’ anasema Rosheda Muller, mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara nchini humo.

Serikali ya nchi hiyo imeyanyooshea kidole cha lawama maduka hayo kwa kusababisha vifo vya watoto hivyo.

Kufuatia shinikizo kubwa kutoka kwa umma, Rais wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa alilazimika kutengeneza kanuni za udhibiti wa maduka ya aina hiyo ndani ya siku 21. Kulingana na Ramaphosa, maduka hayo yanapaswa kuzingatia kanuni muhimu za afya.

Duka la Spaza katika kitongoji kimoja nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema kuwa tatizo ni kubwa kuliko serikali inavyodhani, kufuatia tahadhari mbalimbali zilizotolewa kuhusu udhibiti wa viatilifu na na magenge ya vyakula.

‘’Kama haihusiani na maduka ya spaza, kwanini sasa ni rika fulani tu la watoto wanaougua na sio watu wazima," anahoji Dkt Coetzee.

Utafiti uliofanywa nchini humo na kutolewa mwaka 2023 unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya vifo vya watoto katika kipindi cha miaka 10, vilitokana na sumu ya viatilifu.

‘’Serikali na idara zote za afya zinapaswa kuwa wazi wa kushughulikia suala hili,’’ anapendekeza.

Maofisa usalama wakiwa katika eneo la Naledi, kwenye jimbo la Soweto kwa ajili ya uchunguzi wa maduka ya Spaza.

Sakata la maduka ya spaza limekuwa jambo kubwa kwa sasa nchini Afrika Kusini. Mwezi uliopita, watoto kadhaa walipoteza maisha katika eneo la Naledi katika jimbo la Soweto baada ya kununua vitafunwa katika maduka hayo, tukio lililoibua vurugu kubwa katika eneo hilo.

Huku mikasa ya vyakula kuwa na sumu ikiwa imethibitishwa kwa muda miezi mitatu iliyopita, hatua ya serikali ya kudhibiti sekta hiyo inaonekana kuchelewa.

Vigezo vya usajili wa biashara hizo vinamtaka mmiliki awe raia wa Afrika Kusini huku biashara hiyo ikiwa imesajiliwa na manispaa ya eneo hilo.

Hata hivyo, bado kuna wasiwasi iwapo kama vigezo hivyo vitazingatiwa kwa wakati.

‘’Maduka haya ni kama uhai wa jamii za maeneo, ila kuna umuhimu wa kuyadhibiti na kuwepo mazingira wezeshi ya kuyaendesha. Hata hivyo, ni vigumu sana kutekeleza mambo yote hayo ndani ya siku 21. Tumemuandikia Rais barua, tukimuomba muda zaidi,’’ Muller alisema.

‘’Watupe angalau mwaka mmoja kwa sababu manispaa hazina uwezo wa kusajili wafanyabiashara wasio kwenye sekta rasmi. Kuna mamilioni ya wafanyabiashara wa aina hiyo nchini Afrika Kusini huku wengi wao wakimiliki maduka ya spaza,’’ anaongeza.

Wataalamu wa afya, hata hivyo, wanasema kanuni iliyopendekezwa inaweza isifae katika kushughulikia janga hilo.

‘’ Kwa sasa, msisitizo wote uko kwenye maduka hayo pekee. Wakaguzi wa afya na usalama walikuwa wapi miaka michache iliyopita? Je, walifanya kazi yao,’’ anahoji Dkt Coetzee.

TRT Afrika