Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, imetoa hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wake Ulinzi Yoav Gallant.
ICC iko mjini The Hague, Uholanzi na ilianzishwa Julai 17, 1998, chini ya Mkataba wa Roma, mkataba wa kimataifa, na ulianza kutumika Julai 2002.
Kulingana na Mahakama ya ICC, baada ya kukusanya ushahidi na kumtambua mshukiwa, upande wa Mashtaka unawataka majaji wa ICC kutoa hati ya kukamatwa kwa mtuhumiwa na ICC inategemea nchi kusaidia katika utekelezaji wa agizo hilo.
"Kama taasisi ya mahakama, ICC haina jeshi lake la polisi au chombo cha kutekeleza sheria; hivyo, inategemea ushirikiano wa nchi duniani kote kwa ajili ya kuungwa mkono, hasa kwa kukamata washukiwa, na kuwahamisha hadi ICC huko The Hague, kufungia mali za washukiwa, na kutoa hukumu," imefafanua ICC katika tovuti yake.
Wanachama wa ICC
Nchi 124 ni nchi Wanachama wa Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC.
Kati yao 33 ni mataifa ya Afrika, 19 ni Asia-Pacifiki, 19 ni kutoka Ulaya Mashariki, 28 ni kutoka Amerika ya Kusini na Caribbean, na 25 ni kutoka Ulaya Magharibi na mataifa mengine.
Hata hivyo Marekani, China, India, urusi na Israel si wanachama wa ICC.
Kesi thelathini na mbili zimefikishwa katika mahakama hiyo, ambayo ina majaji 18 wanaotoka nchi tofauti, ambao huchaguliwa na nchi wanachama na kutumikia mihula ya miaka 9, isiyoweza kuongezeka.
Majaji wametoa hati 59 za kukamatwa kwa watu tofauti, zikiwemo zile za sasa za Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu.
Mnamo Machi 2023, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa tuhuma za uhalifu wa kivita katika vita dhidi ya Ukraine.
Watu 21 wamefika mbele ya ICC na kuzuiliwa katika kituo chake. Majaji wa ICC wametoa hukumu 11 na kuachilia watu 4, kulingana na mahakama hiyo.
Mashtaka dhidi ya watu saba yametupiliwa mbali kwa sababu ya vifo vyao.
"Watu 30 bado wako huru," ICC inasema.
Waafrika waliokamtwa ambao wako ICC
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman alihamishiwa chini ya ulinzi wa ICC tarehe 9 Juni 2020, baada ya kujisalimisha kwa hiari katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Taarifa za mwisho za kesi hiyo zimepangwa kuanzia tarehe 11 hadi 3 Desemba 2024.
Hati ya kukamatwa kwa Al Hassan Ag Abdoul Aziz Ag Mohamed Ag Mahmoud ilitolewa tarehe 27 Machi 2018. Alijisalimisha kwa ICC tarehe 31 Machi 2018. Yuko chini ya ulinzi wa Mahakama.
Mnamo tarehe 8 Julai 2019, Mahakama ya ICC ilimpata Bosco Ntaganda na hatia ya makosa 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, uliofanywa huko Ituri, DRC, mwaka wa 2002-2003.
Tarehe 7 Novemba 2019, Bosco Ntaganda aliyejulikana kwa jina la " terminator" alihukumiwa jumla ya miaka 30 jela. Muda aliokaa kizuizini ICC - kutoka 22 Machi 2013 hadi 7 Novemba 2019 - utaondolewa kwenye hukumu hii.
Hati ya kukamatwa kwa Dominic Ongwen, Kamanda wa Brigedia Sinia wa kikundi cha waasi Uganda cha Lord's Resistance Army (LRA), ilitolewa Julai 8, 2005
Mnamo tarehe 21 Januari 2015, Dominic Ongwen alihamishwa hadi katika Kituo cha Kizuizi cha ICC huko The Hague.
Alishtakiwa kwa makosa 70 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika kambi ya wakimbizi Kaskazini mwa Uganda. Kesi yake ilifunguliwa tarehe 6 Disemba 2016.
Tarehe 4 Februari 2021, Mahakama ya ICC ilimpata Dominic Ongwen na hatia 61 zinazojumuisha uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita, uliofanywa Kaskazini mwa Uganda kati ya 1 Julai 2002 na 31 Desemba 2005.
Tarehe 6 Mei 2021, Mahakama hiyo ilimhukumu Dominic Ongwen hadi miaka 25 jela. Mnamo tarehe 18 Disemba 2023, Ongwen alihamishwa hadi Norway kutumikia kifungo chake gerezani.
Hati ya kukamatwa kwa Mahamat Said Abdel Kani anayejulikana pia kama "Mahamat Said Abdel Kain" na "Mahamat Saïd Abdelkani" ("Bwana Said") ilitolewa mnamo 7 Januari 2019.
Anashitakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu unaodaiwa kufanywa huko Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mwaka wa 2013.
Said alijisalimisha kwa ICC tarehe 24 Januari 2021 na kesi yake bado inaendelea.
Amri ya kukamatwa kwa Alfred Yekatom ilitolewa tarehe 11 Novemba 2018. Alijisalimisha kwa ICC tarehe 17 Novemba 2018 na alifikishwa kwa mara ya kwanza mbele ya Chumba cha Utangulizi mnamo 23 Novemba 2018.
Amri ya kukamatwa kwa Patrice-Edouard Ngaïssona ilitolewa tarehe 7 Disemba 2018. Alikamatwa na serikali ya Ufaransa tarehe 12 Disemba 2018 na kuhamishiwa katika kituo cha kizuizini cha ICC tarehe 23 Januari 2019.
Wanashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. Taarifa za kufunga kesi yao kutoka kwa mahakama na mashahidi zimepangwa tarehe 9-12 Disemba 2024.