Ndege iliyobeba mwili wa mwanafunzi huyo, ilikuwa ikitokea uwanja wa kimataifa wa Amsterdam, Uholanzi ilitua katika uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro.
Mazishi ya mwanafunzi huyo yamepangwa kufanyika siku ya Jumanne baada ya maombi huko wilayani Rombo, Kilimanjaro, Kaskazini mwa Tanzania ilipo familia ya marehemu.
"Kifo chake ni hali ngumu kwetu, lakini tunakabiliana nacho," Christina Mtenga, ndugu wa Felix Mtenga aliiambia AFP.
"Clemence alikuwa mwenye adabu, mwenye bidii, mtu wa dini aliyewapenda watu wengine," Christina aliongeza.
Aidha, imekuwa ni mwezi wa kuomboleza kwa familia ya marehemu, kwani Mtenga alitarajiwa kushiriki hafla ya mahafali na kukamilisha shahada yake kutoka chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine nchini Tanzania.
Mwanafunzi huyo wa kilimo, kutoka Tanzania, mwenye umri wa 22, ni miongoni mwa waliouawa kutokana na mashambulio kati ya Hamas na Israel mnamo Oktoba 7.
Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, ingawa imethibitisha kifo cha Mtenga katika taarifa yake iliyoitoa Novemba 18, haikufafanua jinsi alivyouawa.
Shambulio hilo lilitokea mwezi mmoja tu baada ya Felix kuwasili Israel ambapo alitarajiwa kukaa nchini humo kwa mwaka mmoja.
Mtenga na mwanafunzi mwenzake wa Tanzania, Joshua Mollel, 21, walikwenda Israel mwezi Septemba kwa ajili ya mafunzo ya kilimo lakini wote wawili walipotea baada ya shambulio la oktoba 7.
Baada ya uvamizi huo, ubalozi wa Tanzania nchini Israeli ilitangaza kutoweka kwa raia wake wawili nchini humo.
Hatimaye, mwili wa Mtenga ulipatikana baadaye na kutambuliwa baada ya zaidi ya wiki moja, ambapo serikali ya Tanzaniana kupitia ubalozi wake Israeli, ulisaidia kuthibitisha utambulisho wake.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania imesema katika taarifa yake wiki iliyopita kwamba Mollel bado hajapatikana.