Serikali ya Tanzania imetoa Msaada wa Kibinadamu wa Dola za Kimarekani Milioni Moja kwa Uturuki kwa ajili ya walioathirika na tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo tarehe 6 Februari mwaka huu.
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mheshimiwa Lt Jenerali (Mst) Yacoub Hassan Mohammed, amekutana na Mkurugenzi Mkuu Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, AFAD, Muhammet Maruf Yaman, ambapo alikabidhi fedha za Misaada ya Kibinadamu katika makao makuu ya AFAD, Ankara, Uturuki.
Kwa mujibu wa Ubalozi, Tanzania na Uturuki wana ushirikiano mzuri wa kidiplomasia kwa kuzingatia msingi na historia ya udugu. Ni kwa sababu hii kwamba kuna Ubalozi huko Ankara.
“Nchi hizi mbili zinafanya kazi pamoja katika nyanja nyingi, ikiwa ni pamoja na uwekezaji, sekta ya afya, utalii, elimu na utamaduni. Kwa ushirikiano wa aina hii, hakuna sababu kwa nini wasingetoa mkono wa kusaidia”, Ubalozi uliongeza.
Tanzania imesema kuwa inaitazama Uturuki kama “All weather friends” yani marafiki katika jua na mvua, na ikaona hii ni fursa kwa nchi hiyo kudhihirisha ushirikiano wao kwa namna ambayo haiangalii nani ni nchi yenye nguvu zaidi kiuchumi bali kusaidiana katika nyakati nzuri na mbaya.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, na ubalozi huo waliona ni muhimu kuchangia kiasi fulani ili kusaidia kwa namna yoyote ile katika nyakati hizi za changamoto.
"Kutokana na tetemeko, watu wengi sana wamepoteza maisha, huduma za kijamii zimekwama, miundombinu imeharibiwa, watu hawana kazi, na wanawake na watoto wanapambana na hali ya hewa ya baridi." Ubalozi ulisema.
Uturuki na Syria zilikumbwa na tetemeko la ardhi la 7.8 kwenye kipimo cha Richter mwezi Februari. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kukabiliana na Majanga na Dharura ya Uturuki (AFAD), watu 44,208 wamepoteza maisha.
Majengo 173,000 yameporomoka au kuharibiwa vibaya, huku zaidi ya watu milioni 1.9 wamekimbilia makazi ya muda, hoteli na makazi yasiyo rasmi kutokana na tetemeko hio.