Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB Dkt Akinwumi Adesina/  Picha ya AFDB

Rais wa Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika, African Development Bank, AfDB Dkt. Akinwumi Adesina, ameonya kwamba ushuru mpya wa kaboni wa ulaya unaweza kukandamiza kwa kiasi kikubwa maendeleo ya biashara ya Afrika.

Ameonya kuwa ushuru huo utaathiri ukuaji wa viwanda kwa kuwekea vikwazo bidhaa kutoka Afrika ikiwemo mauzo ya nje yaliyoongozewa thamani ikiwa ni pamoja na chuma, saruji, chuma, alumini na mbolea.

Adesina amesema haya katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya tabia nchi, COP28 unaofanyika mjini Dubani katika Falme za kiarabu,

"Kutokana na upungufu wa nishati barani Afrika na kutegemea zaidi nishati ya mafuta, hasa dizeli, maana yake ni kwamba Afrika italazimika kuuza bidhaa ghafi tena Ulaya, jambo ambalo litasababisha zaidi uchumi wa Afrika kudorora, " Adesina amesema.

"Afrika inaweza kupoteza hadi dola bilioni 25 kwa mwaka kama matokeo ya moja kwa moja ya Utaratibu wa Marekebisho ya Ushuru wa Mipaka ya Kaboni ya EU," rais wa Benki ya AfDB aliwaambia wajumbe katika Mkutano wa Biashara Endelevu wa Afrika uliofanyika katika mikutano ya COP28.

“Afrika imebadilishwa kwa muda mfupi na mabadiliko ya hali ya hewa, sasa itakuwa na mabadiliko ya muda mfupi katika biashara ya kimataifa,” rais wa benki alisema.

"Kwa sababu ya ushirikiano hafifu kimataifa, fursa bora zaidi ya biashara barani Afrika ziko katika mabadilishano ya kikanda, huku Eneo jipya la Biashara Huria la Bara la Afrika likikadiriwa kuongeza mauzo ya nje ya Afrika kwa zaidi ya 80% ifikapo 2035."

Adesina alisisitiza kuwa Afrika tayari ilikuwa inapuuzwa katika mpito wa nishati duniani, hayo ni kutokana na takwimu kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nishati Mbadala.

"Afrika ilipokea tu dola bilioni 60 au 2% ya uwekezaji wa dola trilioni 3 wa nishati mbadala katika miongo miwili iliyopita, hali ambayo sasa itaathiri vibaya uwezo wake wa kusafirisha bidhaa kwa ushindani barani Ulaya," Adesina alisema wakati akitoa wito wake.

Wataalamu wanasema Afrika itahitaji kutumia gesi asilia kama nishati ya mpito ili kupunguza utofauti wa nishati mbadala na kuleta utulivu katika mifumo yake ya nishati ili kusaidia ukuaji wake wa viwanda.

TRT Afrika