Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt Akinwumi Adesina amesema kuwa uhaba wa nishati ya umeme unachangia kuporomoka kwa uchumi wa bara la Afrika.
Kulingana na Dkt. Adesina, kutokuwa na nishati ya umeme wa uhakika barani Afrika, kunapelekea kupungua kwa pato la bara hilo kwa asilimia nne, kila mwaka.
"Idadi ya watu wanaoishi bila nishati ya umeme imeongezeka kutoka asilimia 39 kwa mwaka 2015 hadi kufikia 52 ilipofika mwaka 2024," amesema Dkt Adesina wakati wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika, jijini Dar es Salaam, Tanzania Januari 28, 2025.
Kulingana na Dkt. Adesina, AfDB imesaidia zaidi ya watu milioni 25 barani Afrika kufikiwa na nishati ya umeme.
Hata hivyo, licha ya hatua hiyo, bado watu milioni 571 barani humo hawana uhakika na nishati ya umeme, kiwango ambacho ni sawa na asilimia 83 ya watu wanaoishi bila umeme duniani.
"Zaidi ya hayo, watu wengine bilioni moja hawatumii nishati safi za kupikia, hali inayoathiri afya ya akinamama na watoto," ameongeza Dkt. Adesina.
Rais huyo wa AfDB pia amewataka viongozi wa Afrika kufanya jitihada kuhakikisha kuwa idadi hiyo inapunguzwa kupitia mradi wa 'Mission 300', unaolenga kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme wa kwa watu milioni 300 barani Afrika, ifikapo mwaka 2030.