Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Kenya imeanza maombolezi ya siku tatu kufuatia vifo vya watoto 21 vilivyotokea Septemba 5, 2024, baada ya bweni la Shule ya Hillside Endarasha kuungua huko Kieni, Nyeri.
Uchunguzi wa vinasaba yani DNA unaanza hii leo ili kutambua miili ambayo imeshindwa kutambuliwa hapo awali.
Mpaka sasa, kuna wanafunzi wengine 70 ambao hawajulikani walipo.Wakati machozi ya ajali ya Hillside hayajakauka kwa taifa la Kenya, tayari, kumeripotiwa ajali nyengine za moto tatu katika shule nyengine.
Hizo zimetokea katika Kaunti ya Pokot Magharibi mwa nchi, ambapo moto ulizuka katika Shule ya Upili ya Vijana ya Ortuma, ajali nyengine imetokea katika bweni la shule ya upili ya vijana ya Njia eneo la Meru na ya tatu ni Shule ya Upili ya Wasichana ya Isiolo.
Ingawa mpaka sasa hakuna madhara yaliyoripotiwa katika ajali hizi.
Lakini chanzo cha moto katika shule ni nini?
Ni kizungumkuti ambacho sasa kimezua mjadala wa ripoti ambayo Mkaguzi Mkuu wa Seriklai alitoa mwaka 2020 akiashiria kuwa kuna mapengo makubwa ya usalama katika uendeshaji wa baadhi ya shule.
Wizara ya Elimu nchini Kenya mnamo 2008 ilitoa miongozo ya viwango vya usalama kwa shule ili kuhakikisha kuwa shule zinajiandaa kushughulikia ajali za moto iwapo zitatokea.
Hata hivyo, mwaka 2020 Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, yaani Auditor General alitoa ripoti iliyoonyesha utekelezaji wa mapendekezo ya hatua za usalama bado ni duni.
Ripoti hiyo iliweka wazi kwamba, baadhi ya shule hazikuwa na miundombinu ya kutosha ya kupambana na majanga ya moto.
Baadhi ya shule hazikuwa na maeneo maalumu ya wanafunzi kukusanyika iwapo moto utatokea, hivyo kusababisha mtawanyiko wakati wa ajali na kusababisha madhara makubwa.
Masharti yanasema madarasa na bweni lazima ziwe na milango ambayo inafunguka kuelekea nje ili kurahisha watoto kujiokoa wakati wa moto.
Mabweni ya shule yanafaa kuwa na milango kila mwisho wa jengo na madirisha ambayo sio ya chuma.
Uchunguzi ulionyesha kuwa, baadhi ya shule kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ni changamoto ambayo inasababisha mabweni kujaa.Na katika bweni, kunatakiwa kuwe na kitanda kimoja kimoja au kwa ngazi moja tu, lakini kuna shule ambazo zina vitanda vya ngazi mbili.
Mbali na changamoto za miundombinu, baadhi ya ajali za moto zimekuwa zikisababishwa na wanafunzi ambao wana tabia za uhalifu ambao baadhi wameshtakiwa kwa mauaji.
Visa vyengine vimesababishwa na hitilafu za umeme.Ajali nyingi za moto vimekuwa zikitokea katika shule za upili, lakini janga la sasa la shule ya Endarasha katika kaunti ya Nyeri, ni shule yenye takriban wanafunzi 800 wenye miaka kati ya 5 na 12.
Na swali ni, je baada ya kutokea kwa ajali hizi, mapendekezo ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali yatazingatiwa?