Coletta Wanjohi
Kenya imekamilisha makubaliano na kampuni ya Moderna kuanzisha kiwanda cha thamani ya dola bilioni 65 jijini Nairobi cha kuzalisha chanjo.
Moderna ni kampuni ya kibayoteknolojia inayozalisha matibabu na chanjo za Messenger ribonucleic acid, au mRNA kwa ufupi. mRNA ni molekuli yenye ncha moja ambayo hubeba kodi maalum za kijeni kutoka kwa DNA hadi kwa mashine ya kutengeneza protini ya seli.
“Tumefurahishwa na hatua hii muhimu ambayo inatusaidia kuweka wazi juhudi zetu kama serikali kudumisha mtindo wetu wa kiuchumi wa kuwezesha kutoa chanjo sio kwa Kenya tu bali pia bara la Afrika," rais wa Kenya William Ruto alisema.
Mkataba wa maelewano kati ya Kenya na Kampuni hii ya kimataifa ya chanjo ulitiwa saini Machi 2022 na kushuhudiwa na aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.
“Tunatumai kuleta uvumbuzi huu wa kutengeneza chanjo kwa njia ya kiteknolojia inayoitwa mRNA kwa watu wa Afrika katika maeneo yenye mahitaji makubwa, kama vile magonjwa ya maambukizi ya kupumua na magonjwa mengine ya uambukizaji kama ukimwi na zingine kama Zika na Ebola," Stéphane Bancel, Afisa Mkuu Mtendaji wa Moderna alisema.
Kenya inaungana na Rwanda kuanzisha viwanda vya kuzalisha chanjo.
Nchini Rwanda kampuni ya bayoteknolojia yenye makao makuu yake nchini Ujerumani, BioNTech, inajenga kiwanda chake cha kwanza cha kutengeneza chanjo cha mRNA.
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika, NEPAD, linasema Afrika inaripotiwa kutengeneza takriban asilimia 0.1 tu ya chanjo duniani, na bado inaagiza kutoka nje karibu asilimia 99 ya chanjo za magonjwa, na zaidi ya asilimia 95 ya dawa.
Uzalishaji wa chanjo katika viwango tofauti unafanyika nchini Tunisia, Misri, Ethiopia Afrika Kusini na Senegal.
Walakini, janga la COVID -19 lilifichua umuhimu wa Afrika kuwekeza zaidi katika utengenezaji wake wa chanjo. Nchi zimelazimika kusubiri usambazaji wa chanjo ya COVID-19 kutoka mataifa yaliyoendelea.