Uhaba wa maji umeathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za ukulima katika eneo la Sahel. Picha: AFP

Na Firmain Eric Mbadinga

Simulizi hii inaibua hofu kubwa kuhusu hali ya baadaye iliyotawaliwa na kila aina ya majanga yasiyofikirika.

Katika muktadha wa mabadiliko ya tabia nchi, huo ndio ukweli halisi ambao kila mwanandamu anapaswa kukubaliana nao.

Hali ya joto kali lililotawala mwaka uliopita ilisababisha misitu kushika moto na ongezeko la ukataji miti duniani.

Katika jimbo la California nchini Marekani, Zebaki ilifikia nyuzi joto 54 wakati kwa Morocco iligonga nyuzi joto 50.

Kwa zaidi ya miaka 15 sasa Kambamboli Tankoano kutoka Burkina Faso, amejishughulisha na ufugaji na kilimo cha Soya, kijijini kwao Ountandeni.

Kwake yeye, kilimo ni suala la kufa na kupona, pamoja na changamoto ziletwazo na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kambamboli Tankoano akiwa katika shamba lake la Soya, katika kijiji cha Ountandeni nchini Burkina Faso. /Picha: TRTAfrika

Mara kwa mara, Tankoano ambaye anaongoza chama cha ushirika cha wakulima na wafugaji wa ndani, amekuwa akijiweka karibu na taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa zinazotokana na El Niño, na hivyo kuzorotesha shughuli za kiuchumi.

"Tumeanza kuona na kuhisi kupungua kwa msimu wa uzalishaji na hivyo tunalazimika kubadilisha aina ya mazao ya kupanda kutokana na kuongezeka kwa magonjwa ya mimea," anaiambia TRT Afrika.

Mkulima huyo, pia anabainisha anguko la uzalishaji, kuanzia mwezi Julai 2023, ambao kulingana na mamlaka ya hali ya hewa ulimwenguni, unaashiria kuanza kwa madhara yatokanayo na mvua za El Niño.

“Mara kwa mara, tumeshuhudia vipindi virefu vya ukame, vikiambatana na kukauka kwa vyanzo vya maji. Pia tunakumbuna na vikwazo katika uzalishaji wa nje ya msimu na upotevu wa maliasili wakati mifugo yetu inataabika kutokana na ukosefu wa nyanda za malisho," anafafanua.

Athari mbalimbali

Kulingana na Ndague Diogoul, mtafiti wa mambo ya bahari nchini Senegal, kuna tofauti za madhara ya mvua za El Niño, kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Kwa mfano, kwa upande wa eneo la Sahel, madhara hayo hutawaliwa na hali ya nusu ukame. Mabadiliko ya namna hii, pia yanaweza kuongeza vipindi vya ukame, na kuathiri upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji na kunyweshea mifugo.

Ongezeko la hali ya joto kwenye bahari ni ushuhuda wa mabadiliko ya tabia nchi duniani./Picha: AFP

Diogoul anasema kuwa uhaba wa vyanzo vya maji katika eneo la Sahel ambalo pia ni sehemu ya Burkina Faso, unasababisha shinikizo kubwa kwa wakulima na wafugaji wa nchi hiyo.

"Ukame una athari kubwa kwenye aina ya majani na hivyo kuwafanya wafugaji kuhangaika katika kutafuta malisho yaliyo bora. Vilevile, kutofautiana kwa aina za mavuno kunasababisha hali ya usalama wa chakula," anaiambia TRT Afrika.

Uhaba wa maji

Moja ya viashiria vya mabadiliko ya tabia nchi ni ongezeko la hali joto kwenye bahari, kwa mujibu wa jukwaa la mazingira, lijulikanalo kama Planète Mer.

"Mbali na hayo, mimeo asili hupata ushindani kutoka kwa mimea vamizi," anasema Diogoul. "Tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa samaki jamii ya Sardinella wamebadili mtindo wao na mzunguko wa maisha kutokana na mabadiliko yanayotokea katika ukanda wetu."

Kuongezeka kwa kiwango cha joto kwa mwaka 2023, kulishuhudiwa sehemu nyingi duniani.

Mabadiliko haya, hayakuliacha salama eneo la Afrika ya kati. Boris Efoua Aba'a, mfugaji kutoka Libreville, Gabon, alikutana na changamoto nyingi kutokana na hali hii. "Tuligunda kuwa hali ya joto lilidumu kwa zaidi ya miezi minne, tofauti na kawaida," anaeleza.

Uhaba wa maji nao umeendelea kuleta shida kwa wakazi wa maeneo ya vijijini. "Wanyama wetu wanapata adha ya kiu kwani visima vingi vimekauka, kama ilivyo kwa chakula, maji pia ni kitu muhimu sana katika shughuli za ufugaji," anasema Boris.

Hali hii, pia imepelekea kushuka kwa viwango vya mazao yatokanayo na mifugo kama vile nyama, na hivyo kuathiri mapato ya wafugaji hao.

Hofu ya Ubashiri

Mataifa mengi duniani, ikiwemo Gabon ni sehemu yanaakisi uhalisia wa madhara ya El Niño. Kulingana na tafiti zinazoendelea kufanyika,hali inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na mabadiliko ya vipindi vya mvua, hali itayakayosababisha athari kubwa kwenye kilimo.

"Misitu itaendelea kushika moto kutokana na hali mbaya za hewa, na hivyo kuathiri viumbe hai na mifumo yao ya Ikolojia," Diogoul anasema.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa(FAO) limeandaa rasimu na mkakati wa kupunguza madhara ya El Niño katika usalama na uhakika wa upatikanaji wa chakula, hasa kwa watu walio hatarini zaidi.

Kupitia mradi wake unaogharimu dola milioni 160, FAO inalenga kuimarisha kingo za mito ili kupunguza madhara ya mafuriko, kuwalinda wavuvi dhidi ya dhoruba, kutoa mbegu zinazostahimili ukame kwa wakulima na kuandaa dawa za kutosha kwa ajili ya mifugo. Hata hivyo, kiasi kingine cha dola milioni 125, kinahitajika kufanikisha lengo hilo.

Shirika hilo, pia limeweka vipaumbele katika nchi 34 za Afrika, Asia, Pasifiki, Amerika ya Kusini na visiwa vya Caribbean, huku ikiazimia kuwafikia watu milioni 4.8, ifikapo Machi mwaka 2024.

TRT Afrika