Chama Kikuu cha upinzani nchini Ugiriki chataka kutambuliwa kwa dola ya Palestina

Chama Kikuu cha upinzani nchini Ugiriki chataka kutambuliwa kwa dola ya Palestina

Mataifa ya Magharibi yameshindwa kuvumilia kinachoendelea Gaza, amesema kiongozi wa chama hicho.
Chama cha SYRIZA cha nchini Ugiriki kimetaka kutambuliwa kwa dola ya Palestina./Picha: Getty

Chama kikuu cha upinzani cha nchini Ugiriki SYRIZA kimeishinikiza serikali ya nchi hiyo kuitambua dola ya Palestina.

“Ni lazima tujifunze kutokana urafiki wa watu wa Ugiriki na Palestina, tukianzia kwa Waziri Mkuu Andreas Papandreou na Yasser Arafat, na leo tuihusishe kwenye sera yetu ya nje.

Ni lini kama sio leo? Upi ni muda muafaka wa kuitambua dola ya Palestina, tukifuata mfano wa Hispania, Ireland na Norway?” alisema kiongozi wa chama hicho, Stefanos Kasselakis, wakati wa mahojiano na kituo cha redia cha Sto Kokkino.

Akizungumzia ziara yake ya West Bank, ambapo alikutana na maofisa waandamizi wa Palestina na watu wa kawaida, alisema kuwa alijulishwa kuhusu mashambulizi ya Israeli huko Gaza.

"Kwa hiyo kile kilichopaswa kuwa haki ya Israeli ya kujilinda dhidi ya Hamas sasa kimekuwa umwagaji damu, mauaji yasiyo na mwisho," Kasselakis alisema, na kuongeza "Ulimwengu wa Magharibi, Ulaya, Ugiriki hauwezi kuvumilia tena kile kinachotokea Gaza.

"Ulaya lazima iwe na mtazamo. Haiwezi kufuata mfano wa Marekani katika mazungumzo yake yote na Israeli na Palestina na nchi za Kiarabu. Ulaya lazima iwe na mtazamo, na mtazamo na shughuli hiyo lazima iwe kwa ajili ya amani," aliongeza.

Israeli imeua takribani Wapalestina 36,000 katika ukanda wa Gaza toka kulivyotokea shambulizi la Hamas Oktoba 7, mwaka jana lililoua watu 1,200.

Miezi saba toka kutokea kwa mashambulizi hayo, eneo kubwa la Gaza limebakia kuwa magofu, kukiwa na vizuizi vya upatikanaji wa chakula, maji safi na dawa.

Israeli imeshtakiwa katika Mahakama ya Haki ya Kimataifa (ICJ), ambayo imeitaka nchi hiyo kusitisha mauaji hayo ya kimbari na kuwezesha upatikanaji wa misaada kwa raia wa Gaza.

TRT Afrika
AA