Chama cha Tigray People Liberation Front, TPLF, nchini Ethiopia kimesema hakitajisajili tena kama chama kipya kama ilivyotakiwa na bunge.
Kiongozi wa chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF) Debretsion Gebremichael alisema tangazo la hivi majuzi, kuruhusu vyama vya siasa vilivyoharamishwa kujiandikisha upya kama mashirika halali, halikidhi matarajio ya chama chake.
Januari 2021 Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Ethiopia (NEBE) ilifuta usajili wa kisheria wa TPLF kama chama cha siasa ikitaja ushiriki wa chama hicho katika "unyanyasaji wa silaha dhidi ya serikali."
Chama cha TPLF, kilikuwa na kipaumbele kwa uongozi wa nchi hiyo kabla ya 2018 wakati Waziri Mkuu wa sasa Abiy Ahmed kuingia usukani. Vita kati ya jeshi la serikali na wanajeshi waliounga mkono TPLF vilizuka nchini humo kati ya jeshi la seriklai na jeshi lililounga mkono chama hicho cha TPLF.
Kulingana na Debretsion, TPLF inatafuta tu kusajiliwa kama chombo halali cha kisiasa, lakini pia kurejeshwa kwa hadhi yake ya kisheria kabla ya vita.
Juni 2024 Bunge liliridhia marekebisho ya 'Uandikishaji wa Uchaguzi, Vyama vya Siasa na Tangazo la Maadili ya Uchaguzi' katika hatua iliyowezesha makundi ya kisiasa yaliyotangazwa kuwa haramu kutokana na kujihusisha na shughuli zisizo za amani kurejesha hadhi yao ya kisheria kuacha vurugu na kukubali kufanya kazi kwa amani.
Chama cha TPLF
Chama cha The Tigray People’s Liberation Front, TPLF, kilianza mwaka wa 1975 kama kikundi kidogo cha waasi Kaskazini mwa Ethiopia. Kuanzia 1989 hadi 2018, kiliongoza muungano wa kisiasa uitwao Ethiopia Revolutionary Democratic Front.
TPLF iliongoza mapambano dhidi ya serikali ya Derg iliyotawala nchi hiyo kwa miaka 17 chini ya Meja Mengistu Haile Mariam.
Serikali hiyo ilipinduliwa mnamo 1991 TPLF iliweka serikali mpya nchini Ethiopia mwaka 1991 na kubakia madarakani.
TPLF iliondolewa kwenye udhibiti wa serikali ya shirikisho mwaka wa 2018 baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutwaa mamlaka.
Tarehe 3 Novemba 2020, vita vilizuka kati ya wanajeshi waliokuwa wanaunga mkono TPLF na wale waliounga mkono serikali kuu.
Mnamo 2021, Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Ethiopia ilifuta usajili wa TPLF kama vuguvugu la kisiasa, ikiishutumu kujihusisha na vita.
Mnamo Mei 6, 2021, bunge la Ethiopia liliorodhesha TPLF kama kundi la kigaidi na tarehe 2 Novemba 2022, Serikali ya Shirikisho la Ethiopia na TPLF zilitia saini mkataba wa amani mjini Pretoria, Afrika Kusini, ili kumaliza mzozo wa miaka miwili Kaskazini mwa Ethiopia.