Na Firmain Eric Mbadinga
Nadharia ya 'Ukuta wa Kijani' iko mbioni kubadilisha taswira ya eneo la Sahel.
Kama nadharia ya kuhuisha bainowai, ikiwa pia ni vuguvugu la kuunganisha jamii katika ustahimilivu wa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Kila mbegu ipandwayo, huwa ni zaidi ya mti.
Miaka 40 baada ya Rais wa kwanza wa Burkina Faso, Thomas Sankara kugusia umhimu wa kuongezeka kwa jangwa la Sahara, wazo la Rais wa zamani wa Senegal Abdoulaye Wade lilirejesha mkakati huo mwaka 2007.
Mradi wa 'Ukuta wa Kijani' umepata msukumo mkubwa, ndani ya miaka michache iliyopita.
Uzingatiaji wa chini
Chad ni kati ya nchi 11 barani Afrika zilizochaguliwa kama mfano wa utekelezaji wa 'Ukuta wa Kijani', mradi ambao unahamasisha jamii kupanda miche mingi iwezekanavyo kuzuia kutokea kwa hatari ya jangwa.
Juhudi za nchi ya Chad zinafanyika katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 7,000 na upana wa kilomita 15 karibu na eneo la Sahel.
Lengo la mradi huo ni kuhuisha mazingira katika eneo linaloanzia Dakar mpaka Senegal, huku ukuta huo ukikamilika ifikapo mwaka 2030.
Taasisi ya ANGMV, iliyoanzishwa mwaka 2012, ndio yenye kutekeleza mradi wa 'Ukuta wa Kijani'.
''Toka kuanzishwa kwake, ANGMV imehusika na kuhuisha zaidi ya hekari 36,000 za ardhi, uzalishaji wa mbegu milioni 2 kupitia mashamba darasa 12 na uchambaji wa visima 76," Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Kodou Choukou Tidjani, anaiambia TRT Afrika.
ANGMV pia ilihusika na kutoa mafunzo kwa jamii za eneo hilo kuhusiana na uhifadhi endelevu wa ardhi na kukuza ushirikiano na mashirika ya kikanda na kimataifa.
Nahadja Basile, Karibu Mkuu wa idara ya Dar-Tama katika jimbo la Wadi Fira, anasema kumekuwepo na tija kutokana na mradi wa ANGMV katika eneo la Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, ambalo lina jumla ya watu 180,000.
"NImejionea mimi mwenyewe umuhimu wa mrahi huu, hususani katika kambi za wakimbizi za Koungou na Mile. Jumla ya watu 250 waliajiriwa kati ya mwezi Juni na Septemba. Mradi wa ANGMV unazijengea uwezo jamii ili kufanikisha uhuhishwaji wa ukijani katika maeneo yaliyokaribia kuwa jangwa," anaeleza.
Kama sehemu ya mradi wa Albiä wenye kufadhiliwa na Benki ya Dunia, taasisi ya ANGMV inaendeleza juhudi zake za uhuhishwaji wa misitu kupitia ufadhili kupitia washirika wa maendeleo kama vile Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Shirika la Mpango wa Chakula duniani, Shirika la Chakula na Lishe la Umoja wa Mataifa. Serikali ya Chad nayo inachangia katika utekelezwaji wa mradi huo.
"Kufikia sasa, kiasi cha miche 130,000 imepandwa. Jamii zimepokea mafunzo ya namna ya kupanda nyasi kwa ajili ya wanyama," Basile anaiambia TRT Afrika.
Vifaa vya kisasa hutumika kuweka mbolea kwenye ardhi zilizoathirika na ukame.
Jamii kama kitovu
Mafanikio ya mradi huu yanatokana na jitihada za Brahim Ali, mwanamazingira aliyeshiriki katika miradi ya aina hii katika eneo la Kanem.
"Niliwasiliana na idara ya taifa wakati wa kampeni hii. Niliamua kujihusisha kama mtu wa kujitolea katika jitihada hizi baada ya kushiriki vikao vingi veyenye kuhusu mradi huu," anakumbuka.
Kando na kusaidia watu wa kujitolea kama vile Brahim Ali kupitia mafunzo, ANGMV hutoa mbegu, zana na miundombinu mingine muhimu, kama vile vitalu, ili kurahisisha kazi shambani.
Tidjani anaamini kufikia malengo yaliyowekwa na wakati na juhudi endelevu ni muhimu kwa mafanikio ya mradi huo.
"Mwaka huu, ANGMV imepanga hatua mahususi kama vile kupanua usaidizi wa upanuzi wa asili, programu za upandaji miti upya karibu na kambi za wakimbizi, na kuongeza uelewa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Sehemu maalum ya ushirikiano na jamii kwa ajili ya usimamizi endelevu wa maeneo pia iko kwenye ajenda," alisema.
Hatua moja baada ya nyingine
Ratiba iliyowekwa na Umoja wa Mataifa ya kukamilika kwa ukuta huo, inaweza kuonekana kuwa ngumu, lakini wale wanaohusika katika mradi huo wanajua kuwa wako kwenye njia muafaka.
Baada ya kukamilika kwake, ukuta huo, sio tu utazuia jangwa, bali pia utadhibiti tani milioni 250 za hewa ukaa, na hivyo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kulingana na Brahim Ali, ni muhimu kwa wakazi wa ndani kushirikishwa na kujitolea kikamilifu kwa ajili ya mradi huo. “Wanahitaji kufahamishwa na kufundishwa umuhimu wa upandaji miti upya huku wakiunganisha kanuni endelevu za usimamizi wa maliasili,” anasema.
Kulingana na wataalamu, programu zaidi za elimu na motisha za kiuchumi, kama vile kukuza kilimo mseto, zinaweza kuhimiza ushiriki zaidi.
"Pia ni muhimu kufuatilia na kutunza mashamba. Kupanda miti ni hatua ya kwanza tu. Mafanikio yetu yanategemea kwa kiasi kikubwa ufuatiliaji wa mara kwa mara," Brahim Ali anaiambia TRT Afrika.
Mawazo haya yanawiana na mapendekezo ya kimkakati yaliyoundwa na taasisi mbalimbali za kimataifa na tayari yametumiwa na baadhi ya majimbo yanayofanya kazi kwenye Ukuta Mkuu wa Kijani.
Kulingana na utafiti wa mwaka 2020, uliofanywa na Shirika la Transparency International, Ethiopia inaongoza katika kufikia malengo hayo.
Nchini Chad, wanaoendesha mradi huo wanasisitiza kuwa hizi ni mbio za marathon, na si mbio fupi. "Ili kuhakikisha matokeo ya ubora mwishoni mwa mradi, ANGMV inachagua kwa uangalifu kila mti kwa ajili ya kupanda," anasema Tidjani.
''Tunahamasisha spishi za ndani kama vile maralfalfa, moringa, acacia, na mbuyu, ambazo zote zimezoea hali ya hewa ya eneo hilo na kunufaisha udongo na jamii za wenyeji. Mimea hii imechaguliwa kwa ajili ya kustahimili ukame, uwezo wa kuboresha rutuba ya udongo, na kutoa mazao ya misitu yasiyo ya mbao."