Serikali ya Chad imemuamuru balozi wa Ujerumani Gordon Kricke kuondoka nchini humo ndani ya saa 48, ilisema katika taarifa yake, bila kutoa sababu maalum ya kufukuzwa.
"Uamuzi huu wa serikali umechochewa na tabia ya kukosa adabu na kutoheshimu desturi za kidiplomasia," Wizara ya Mawasiliano ya nchi hiyo ilisema kwenye Twitter siku ya Ijumaa.
"Hatujawasiliana rasmi," chanzo katika ubalozi wa Ujerumani kiliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina, ambalo lilisema kuwa alisikia habari hizo kupitia mitandao ya kijamii.
Kricke amewahi kuwa mwanadiplomasia huko Niger, Angola na Ufilipino. Pia alikuwa mwakilishi maalum wa Ujerumani katika Sahel isiyokuwa na utulivu.
Chanzo cha serikali kiliiambia AFP, kwa sharti la kutotajwa jina, kwamba Kricke alionekana "kuingilia sana" utawala wa nchi, na kutoa matamshi ya mgawanyiko. Alikuwa ameonywa mara kadhaa, chanzo kiliongeza.