Siku ya Jumatatu, Mahakama hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa inaanza kusikiliza shauri hilo linalotaka kusitishwa kwa misaada ya kijeshi kwa Israel, kwa madai kwamba Berlin 'inawezesha' mauaji ya kimbari na ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa katika eneo la Gaza.
Kesi hiyo inaihusisha moja kwa moja Israel na vitendo vyake dhidi ya Gaza, ingawa ilifungiliwa mahakamani hapo na nchi ya Nicaragua.
“Tumetulia na tutatoa msimamo wetu wa kisheria mahakamani,” Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani Sebastian Fischer amesema kabla ya kuanza kwa shauri hilo.
“Tunapinga madai ya Nicaragua,” Fischer aliwaambia waandishi wa habari mjini Berlin siku ya Ijumaa. “Ujerumani haijakiuka mkataba wa kimbari wala ule wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, tutatoa hoja hizi kwa kina mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki.”
Nicaragua imeiomba mahakama hiyo kutoa maamuzi ya awali ikiwemo ya kuitaka Ujerumani 'kusitisha mara moja kuipelekea Israel misaada, ikiwemo ya kijeshi kwa kuwa ipo kinyume na mkataba wa kimbari' na sheria ya kimataifa.
'Kusitisha usambazaji wa silaha Israel '
Mahakama hiyo itatumia wiki mbili kutoa maamuzi yake kwenye shauri la Nicaragua na kuna uwezekano kuwa litachukua muda mrefu.
Usikilizwaji wa shauri hilo unakuja kufuatia shinikizo la kutaka kusitishwa kwa misaada kwa Israel, huku mashambulizi yake dhidi ya Gaza yakidumu kwa miezi sita sasa.
Mashambulizi hayo yamewaacha watu wengi wa Gaza bila ya makazi, huku kukiwepo baa kubwa la njaa. Kulingana na Umoja wa Mataifa, ni wapalestina wachache walioweza kukimbia eneo hilo.
“Kesi hiyo itaongeza shinikizo zaidi dhidi ya Israel,” amesema Mary Ellen O’Connell, Profesa wa sheria na masomo ya amani katika chuo kikuu cha Notre Dame.
Siku ya Ijumaa, chombo hicho cha Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa ilizitaka nchi kuacha kuiuzia Israel silaha, wala kusafirisha silaha kuelekea nchi hiyo. Hata hivyo, Marekani na Ujerumani zimepinga hatua hiyo.
Pia, mamia ya wanasheria wa Uingereza, wakiwemo majaji watatu wastaafu wa Mahakama ya hiyo ya Juu, wameitaka serikali yao kusitisha kuiuzia Israel silaha baada ya raia watatu wa Uingereza kuwa miongoni mwa wafanyakazi saba wa kutoa misaada kutoka shirika la kutoa misaada la World Central Kitchen waliouawa katika mashambulizi ya Israel. Israel ilisema shambulio dhidi ya wafanyikazi wa misaada lilikuwa kosa lililosababishwa na "kutambuliwa vibaya."
Kwa miongo kadhaa, Ujerumani imeiunga mkono Israel. Siku chache baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, Kansela Olaf Scholz alieleza: “Historia yetu wenyewe na uwajibikaji wetu uliotokana na mauaji ya wa Israel, inatupa sababu ya kutoa ulinzi kwa Israel,” aliwaambia wabunge.