CCM inataka mjadala wa wazi na CHADEMA. Picha/TRT Afrika. 

Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania CCM kimetoa mwito kwa Chama cha upinzania CHADEMA kuandaa mdahalo wa wazi ili kujadiliana hoja zinazokinzana baina ya vyama hivyo viwili juu ya maoni na mabadiliko ya sheria ya uchaguzi.

“Ajenda ya CHADEMA wanataka tuwe na wabunge 740 badala ya 360, badala ya kuja na namna ya kupunguza idadi ya wabunge ili tuwatumikie wananchi na kutatua kero zao, wao wanaongeza na hiyo ni hoja ya yeye (Mbowe) kutaka watu waandamane," amesema Paul Makonda.

Mbali na kupanda kwa gharama za maisha CHADEMA wanailalamikia Serikali kwa madai ya kutozingatia maoni na mapendekezo ya wadau juu ya miswada ya Sheria za Uchaguzi zinazotarajiwa kuwasilishwa Bungeni kwa ajili ya mabadiliko.

Sheria hizo ni pamoja na ile ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2023, Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa Mwaka 2023 pamoja na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) ya Mwaka 2023.

Kutokana na sababu hizo, CHADEMA imedhamiria kuitisha maandamano kwa lengo la kushinikiza kuzingatiwa kwa maoni hayo, hivyo kuibua mjadala mkubwa katika jamii. Maandamano hayo yamepangwa kufanyika wiki ijayo tarehe 24, lakini CCM imetoa wito kwa CHADEMA wa kufanya mdahalo wa wazi utakaojadili hoja hizo kinzani.

“Katika mapendekezo 84 yaliotolewa, mapendekezo 63 yote yamechukuliwa na yapo kwenye muswada ambao hatua za kisheria zinaendelea katika kuundwa kwa sharia,’’ alisema Makonda na kuongeza, "Lakini sivyo tu, Mbowe ni mnufaika mkubwa wa maridhiano yaliomfanya kuwa huru, wagombea au kesi zote za kisiasa zilizokuwa gerezani na mengine mahakamani kuachiwa bila masharti,” aliongeza.

Makonda ameendela kumshutumu mwenyekiti wa Chadema Mbowe kwa kile alichokitaja kwamba ndiye aliyekuwa chanzo cha kukwamisha mchakato wa kulileta taifa pamoja.

“Na wakati tunaingia kwenye mchakato wa katiba hoja ilitolewa kwamba kwa nini tusifanye mabadiliko na tukaingia kwenye mchakato huo kwa kubadili baadhi ya vifungu ikiwemo Tume ya Uchaguzi, wagombea binafsi, lakini Mbowe na timu yake walikataa na wakasema wanataka katiba mpya, matokeo yake hatukukamilisha mchakato wa katiba mpya kwa sababu ya hulka ya kaka yangu Mbowe ya kukimbia mchezoni kabla ya mchezo kuisha,” alisema Makonda.

Hata hivyo maandamano yaliopangwa na Chadema kufanyika kote nchini kwa kuanzia Dar es Salaam huenda yameanza kupata yasifanyike kutokana na mwingiliano wa ratibu baada ya Mkuu wa Mkoa huo Albert Chalamila kutangaza zoezi la kufanyika usafi litakalohusisha vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.

“Kutakuwa na wanajeshi wengi zaidi ya 5000, Polisi zaidi ya 3000, Jeshi la zimamoto 2000, watu wa usalama barabarani, JKT, watu wa uhamiaji lakini katika kufanya usafi kutakuwa pia na magari ya wanajeshi kwa ajili ya kukusanya taka. Kwa hiyo mkiwaona msiogope, labda kama kuna watu ambao wamedhamiria kufanya fujo,” amesema Chalamila.

TRT Afrika