Chama cha Upinzani nchini Tanzania CHADEMA, kimelaani kukamatwa kwa baadhi ya viongozi na wanachama wake katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe muda mrupi tu baada ya taarifa za kukamatwa kwa viongozi wa Baraza la Vijana wa Chadema, BAVICHA kuenea mitandaoni.
"Tunadai kuachiwa haraka na bila masharti kwa viongozi, wanachama na wapenzi wetu wote waliokamatwa maeneo mbalimbali ya nchi," aliandika Mbowe katika ukurasa wake wa X.
Kwa upande wake, msemaji wa Chadema John Mrema, ameithibitishia TRT Afrika, kwamba miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika, Tundu Lissu, Joseph Mbilinyi almaarufu Sugu pamoja na viongozi wengine wa BAVICHA.
Awali taarifa zilisambaa mitandaoni mwishoni mwa juma, zikionyesha baadhi ya viongozi wa Chama hicho wakilalamika kuzuiwa na Jeshi la Polisi wakiwa safarini kuelekea Mbeya katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanayofanyika Agosti 12 ya kila mwaka.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni 'Chukua jukumu kwa maisha yako ya baadae.'
Hata hivyo, Jeshi la Polisi nchini Tanzania, siku ya Jumapili lilitangaza kupiga marufuku maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na vijana kutoka Chama Kikuu cha Upinzani, Chadema kwa madai kwamba, walipanga kufanya vurugu.
"Polisi wameamua kupiga marufuku aina yoyote ya mikusanyiko ya ndani na ya hadhara au maandamano kwa kisingizio cha kuadhimisha siku ya vijana," alisema Awadh Haji, Kamishna wa Jeshi la Polisi anayehusika na operesheni mafunzo.
"Tunadai kuachiwa haraka na bila masharti kwa viongozi, wanachama na wapenzi wetu wote waliokamatwa maeneo mbalimbali ya nchi," amesisitiza Mbowe.