Tayari joto la kisiasa limeanza kupanda nchini Tanzania, ingawa muda rasmi wa kufanya kampeni haujatangazwa, lakini upinzani umeanza kulalamika kwamba chama tawala CCM kimeanza kuzunguka maeneo mbalimbali ya nchi na kukutana na wapiga kura, kwa kisingizio cha kuzindua miradi.
Uchaguzi wa mwaka huu, unatarajiwa kuwa tofauti na ule wa miaka mitano iliyopita, ambapo upinzani ulilalamika kugaragazwa na CCM.
Hii ni baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuja na falsafa inayosisitiza Maridhiano, Mabadiliko, Ustahimilivu na Ujenzi Upya maarufu kama R4.
Ni kupitia falsafa hiyo, ambapo pia aliruhusu upinzani kuendelea na mikusanyiko yao ya hadhara, kama sehemu ya kunadi sera zao kwa wapiga kura, huku akisisitiza siasa za kistaarabu. Hatua ambayo ilisifiwa ndani na nje ya Tanzania.
Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa nchini Tanzania, hususani kutoka Chama kikuu cha upinzani CHADEMA, wameanza kumkosoa Rais Samia na kusema, falsafa yake haina utashi wa kisiasa.
Hii imetokana na kamata kamata ya hivi majuzi ya baadhi ya viongozi wa Chadema na wafuasi wao waliokuwa wanaelekea mkoani Mbeya kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani. Chadema ilipanga kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya maandamano, licha ya marufuku ya polisi.
Miongoni mwa waliolaani ukamataji huo, ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM aliyetaka kuachiliwa kwa viongozi hao, na kuahidi kufanya mazungumzo.
Inasemekana kuwa, hii itakuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya CCM kutoa wito wa kuachiwa kwa viongozi wa upinzani. Je, hii inaashiria nini? Ni muendelezo au utekelezaji wa R4 za Rais Samia?