Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Freeman Mbowe pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara Tundu Lissu wamekamatwa mapema hii leo.
Chadema imeiambia TRT Afrika kwamba Lissu amekamatwa akiwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kupelekwa kituo cha polisi Mbweni, huku Mbowe amekamatwa akiwa Magomeni.
CHADEMA pia imethibitisha kupitia taarifa kuwa miongoni mwa waliokamatwa pia ni Dkt. Lillian Mtei , mke wa Freemnan Mbowe, na Nicole Freemna Mbowe mtoto wake,
Viongozi wengine waliokamatwa ni Benson Kigalia ambaye ni naibu katibu Mkuu bara, Godbless Lema ambaye ni mwenyekiti wa chama kanda ya kaskazini.
Rhoda Kunchela na Emmanuel Ntobi wenyeviti wa chama mikoa ya katavi na Shinyanga pia wameripotiwa kukamatwa.
Taarifa ya chama inaongezea kuwa viongozi mbali mbali wa majimbo ya kanda ya chama, wanachama zaidi ya 40 na walizni na watumishi wa ofisi waliokuwa ofisini walikamatwa pia.
Kukamatwa kwa viongozi hawa wa upinzania nchini Tanzania, kunakuja muda mfupi kabla ya kuanza kwa maandamano yaliyoitishwa na chama hicho, yakipinga kile wanachodai, utekaji nyara unaoendelea nchini humo, ambao unadaiwa kufanywa na watu wasiojulikana.
Hivi karibuni, CHADEMA ilimpoteza mmoja wa viongozi wake Ali Mohamed Kibao ambae alitekwa akiwa katika usafiri wa umma na hatimae mwili wake kupatikana umetupwa jijini Dar es Salaam akiwa na dalili za kuteswa na kumwagiwa tindi kali.
“Makamu Mwenyekiti ameshaanza kuandika maeleozo kituo cha polisi Mbweni. Anatuhumiwa kutenda kosa kinyume na kifungu Na. 390 cha Sheria ya Makosa ya Jina kama ilivyorekebishwa mwaka 2022,” amesema John Mrema, Katibu Mwenezi wa chama hicho.
Hata hivyo, maandamano hayo yanafanyika wakati ambapo, polisi nchini humo inadai haijatoa kibali, na hivyo kutahadharisha umma.
“Hakuna maandamano, na watakaothubutu kuandamana watakiona,” katika mahojiano yake na moja ya chombo cha habari nchini humo, amesema Muliro Jumanne Muliro, ambaye ni kamanda wa kanda maalumu ya Dar es Salaam.
Kwa upande wake, chama kingine cha upinzani ACT Wazalendo kilitoa wito hapo jana kwa CHADEMA kuahirisha maandamano hayo ili kutoa fursa wa mazungumzo kufanyika.
Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan ameketea vitendo vya uvunjifu amani humo na kusema, katu serikali yake haitafumbia macho vitendo hivyo.
Kufikia kuchapishwa ripoti hii Jumatatu asubuhi, polisi hawajatoa maelezo yoyote kuhusu kukamatwa kwa viongozi hao.