Bunge la Kenya litaanza kuwahoji makatibu wa baraza, sawa na mawaziri walioteliwa na Rais William Ruto huku akibadilisha safu ya uongozi wake.
Rais amependekeza majina 20 ya makatibu wa baraza baada ya kutengua baraza lake la hapo awali kufuatia maandamano yaliyoongozwa na Gen Z tangu Juni 2024.
"Kamati ya uteuzi itaendesha vikao vya kuidhinisha au kuwahakiki wateule kuanzia tarehe 1 hadi 4 Agosti katika ofisi za jengo dogo la bunge kuanzia saa mbili za asubuhi ..."bunge imesema katika taarifa kwa umma.
Kila siku majina matano yatajadiliwa.
Rais William Ruto amewarejesha baadhi ya mawaziri waliokuwa katika baraza alilotengua 11 Julai 2024. Kati yao aliyebakisha nafasi yake ya awali ni katibu wa baraza wa Wizara ya Mambo ya Ndani Kithure Kindiki.
Wengine sita wamebadilishiwa wizara.
Rais Ruto pia amewateua waliokuwa katika upinzani kuchukua nafasi katika wizara tofauti.
"Kamati inatarajiwa kuwaarifu waliopendekezwa mara moja nakuanza mikutano ya kuwahoji ndani ya siku 28," spika wa bunge Moses Wetangula alisema bungeni.
Rais bado hajamteuwa mkuu wa sheria.