Na Dayo Yussuf
Tarehe 27 ya kila mwezi, Omar huenda kwa wakala karibu na nyumbani kwake huko Doha ili kutuma pesa kwa mama yake nchini Kenya. Amekuwa akifanya hivi kwa miaka 9 sasa.
‘’Alhamdulillah pesa ninazotuma kwa mama yangu hutumika kulipia huduma na ada fulani kwa mpwa wangu,’’ Omar anasema.
Hili ni jambo linalofahamika sana miongoni mwa mamilioni ya Waafrika wanaoishi na kufanya kazi katika mataifa ya nje. Kujitolea kila wakati kutuma fedha kwa familia na marafiki nyumbani kwa lengo la kuwasaidia kukabiliana na gharama ya maisha ya kila siku.
Na hiyo ni 'Black Tax'.
Kimsingi, 'Black Tax' ilikusudiwa kuwa jambo zuri, licha ya sifa mbaya iliyoiandama.
Hujenga jumuiya na kukuza uimarishaji wa kijamii, lakini pia inaweza kuweka mzigo mkubwa wa kifedha na kuwatatiza wachangiaji.
‘’Wakati fulani unakuta mtu ametuma pesa zake zote kwamba hana pesa za kulipa kodi lakini ametuma pesa nyumbani. Hata ukiwa umetua ng'ambo, au umekuwa huko kwa mwezi mmoja tu, bado haujapata hata viza yako ya kazi, lakini watu bado wanatarajia kuwatumia pesa nyumbani,'' asema Owen Githiga, mshauri wa masuala ya uhamiaji anayeishi Marekani.
Kwa upande mmoja, 'Black Tax' ingetumika kukuza na kuimarisha hali ya maisha ya familia na jamii, kukuza maadili ya kitamaduni kama vile Ubuntu na udugu, na pia inasaidia kukuza elimu na ukuaji mwingine wa kifedha na kiuchumi.
Lakini kwa upande mwingine 'Black Tax' inaweza kuleta shinikizo kubwa la kifedha, haswa kwa wale ambao wanaanza kazi katika mataifa ya kigeni.
Wachangiaji mara nyingi hujikuta hawawezi kuweka akiba kwa malengo ya binafsi, kama vile kununua nyumba, kuwekeza, au kujenga familia zao wenyewe.
Katika baadhi ya matukio, 'Black Tax' inafanya watu washindwe kujitegemea, na kuwafanya wale waliozowea kupokea kubweteka washindwe kuwa huru kifedha. Kutozingatia mipaka au kupunguza matarajio na majukumu kunaweza kusababisha chuki au migogoro ndani ya familia.
Pia matarajio yasiyokoma ya kutuma pesa yanaweza kusababisha mfadhaiko, wasiwasi, na uchovu au msongo wa mawazo.
‘’Kwa bahati mbaya watu wengi hawana ujasiri wa kusema hapana. Kwa hiyo wanaishia kushinikizwa kutuma pesa, wakijaribu kutosheleza mahitaji ya kurudi nyumbani lakini unaishia kuhangaika hapo ulipo. Watu wengi hawajui jinsi ya kufahamisha familia zao, na kuwafanya waelewe kwamba unachodai ni zaidi ya uwezo wangu,’’ Owen anaiambia TRT Afrika. ‘’Unatakiwa kuwaomba wapunguze mahitaji na matarajio, ujijenge kwanza ili uweze kuwajenga na wao,’’ anasema.
Kulingana na wataalamu, msaada wa kifedha unatakiwa kulenga kuwawezesha wapokeaji, kama vile ufadhili wa elimu au kutoa mitaji kwa biashara ndogo ndogo, badala ya kuwafanya waendeshe maisha yao kwa kukutegemea.
Kwa bahati mbaya, watu wengine wanapata funzo hili, kipindi muda umeshakwenda sana, na kwamba jukumu lao la kwanza ilitakiwa watimize mahitaji yao kwanza kabla ya kuwahudumia wengine.
Kuna watu wengi wanaoishi nje ya nchi ambao wanahisi hawawezi kurudi nyumbani, wakati mwingine kwa sababu ya aibu kwamba hawakuwekeza chochote kwa miaka mingi au hawana akiba.
‘’Ukirudi bila akiba yoyote ya muhimu, watu wale wale uliokuwa ukiwasaidia nyumbani watakukosoa kwa kurudi mikono mitupu,’’ anasema Owen.
'Black Tax' ni ishara ya maadili ya jamii, mshikamano na uthabiti, inayochukua jukumu muhimu katika kuinua jamii. Lakini, utumiaji wake usiodhibitiwa unaweza kuharibu msingi na malengo yake asili.