Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania, wafanyabiashara wanahitaji kuwalipisha wakaazi wanaolenga kulipia bidhaa na huduma nchini humo, kutumia shilingi ya Tanzania wala sio fedha za kigeni.
Wafanyabiashara hao wanahitajika kuzingatia tamko la makatazo yaliyotolewa na taifa hilo mnamo mwezi Agosti 2007 na mwezi Desemba 2017
“Siku za karibuni imebainika kuwepo kwa ukiukwaji wa Tamko hilo. Hivyo, Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa kama ifuatavyo”. Taarifa hiyo ilionya.
Raia hao wameonywa dhidi ya kuwatoza wakaazi wake kupitia fedha za kigeni haswa wakati wa kufanya malipo yanayogusa huduma kama vile; kodi za kupangisha ardhi, nyumba na ofisi; gharama za elimu; huduma za afya, vifaa tiba na vitendanishi; gharama za usafiri, lojistiki na bandari; vifaa vya kielektroniki na huduma za mitandao ya mawasiliano na kadhalika.
“Mkaazi yeyote wa Tanzania anapaswa kufanya malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania pekee na hivyo asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni.”
“Mkaazi yeyote wa Tanzania anapaswa kufanya malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania pekee na hivyo asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni.”
Hata hivyo, malipo kama vile gharama za hoteli, usafiri, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania na gharama za mizigo bandarini zimeruhusiwa kutekelezwa kupitia fedha za kigeni.
“Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakaazi, zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni.” Benki hiyo ilifafanua.
Wateja wanaotumia fedha za kigeni sasa watalazimika kujitambulisha kwa stakabadhi muhimu kama hati ya kusafiri na nyaraka za usajili kwa makampuni ikiwa ni katika masharti yaliyowekwa na benki hiyo.
Taarifa iliyosainiwa na Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba, imeonya vikali dhidi ya kutokubali malipo kwa shilingi ya Tanzania, huku ikieleza kuwa ni ukiukaji wa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, kinachoelekeza kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo inaruhusiwa kutumika nchini humo.
Haya yanajiri huku ongezeko la thamani ya fedha za kigeni ikiathiri biashara kata mataifa mbalimbali.