Akiba ya fedha za kigeni nchini Tanzania ilifikia dola bilioni 5.29 mwishoni mwa Julai/ Picha : Reuters 

Mdhibiti wa madini nchini Tanzania ameziagiza kampuni zote za uchimbaji madini na wafanyabiashara wanaosafirisha dhahabu nje ya nchi kutenga angalau asilimia 20 ya bidhaa hiyo kwa ajili ya kuiuzia benki kuu ili kuimarisha hatua ya benki hiyo ya kuweka akiba ya fedha za kigeni.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza kununua dhahabu kutoka kwa wafanyabiashara na wachimbaji madini wa ndani katika mwaka wa fedha uliopita ulioishia Juni ili kuongeza akiba yake huku kukiwa na shinikizo la kushuka kwa thamani ya fedha ya ndani, shilingi.

Katika kipindi cha miezi 12 hadi Juni, benki kuu ilinunua kilo 418 za dhahabu ili kuongeza akiba yake na katika mwaka huu wa fedha inakusudia kununua tani 6 za dhahabu.

Mdhibiti, Tume ya Madini Tanzania, alisema Ijumaa katika taarifa yake kwamba agizo hilo litaanza kutumika kikamilifu Oktoba 1 kama sehemu ya sheria mpya ya madini iliyotungwa.

Wachimbaji na wafanyabiashara, kwa mujibu wa taarifa hiyo, watatakiwa kuwasilisha dhahabu iliyohifadhiwa kwenye viwanda vikubwa viwili vya uchenjuaji madini, Eye of Africa Ltd katika mji mkuu Dodoma na Mwanza Precious Metals Refinery Ltd, vilivyopo Ziwa Mwanza, kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

“Malipo yote yatafanyika kwa mujibu wa utaratibu wa Benki Kuu ya Tanzania,” ilisema taarifa hiyo bila kutoa maelezo ya kina kuhusu viwango.

Akiba ya fedha za kigeni nchini Tanzania ilifikia dola bilioni 5.29 mwishoni mwa Julai, zinazotosha kugharamia miezi 4.3 ya makadirio ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.

Reuters