Wafanyabiashara nchini Ethiopia wanapata afueni katika masharati mapya ambayo yametolewa na Benki kuu ya Ethiopia.
"Ili kukuza jitihada ya mauzo ya nje, hasa kwa wauzaji wa bidhaa za nje, mahitaji ya kujisalimisha kwa fedha za kigeni pia yanapunguzwa," gavana wa benki kuu ya Ethiopia, Mamo Mihretu, benki kuu amesema katika taarifa.
"Agizo jipya linatolewa ambapo wauzaji bidhaa na huduma nje ya nchi watatoa 50% ya mapato yao ya fedha za kigeni kwa Benki ya taifa, NBE, 10% kwa benki zao, na kubakisha 40% kwa akaunti yao wenyewe," Mihretu ameongezea.
Kabla ya masharti mapya wafanyabiashara walitakiwa kusalimisha asilimia 70 ya mapato yao ya fedha za kigeni kwa benki kuu kulingana na kiwango cha kubadilisha fedha kilichokuwepo wakati huo,
Waliruhusiwa tu kubakisha asilimia 20 ya mapato.
Asilimia 10 iliyobaki ilibidi ikabidhiwe kwa benki za biashara.
Hatua hiyo inalenga kuwapa motisha wauzaji bidhaa nje na kuongeza ushindani wa mauzo ya Ethiopia katika masoko ya kimataifa.
Katika masharti mapya pia, kiwango cha riba katika kituo cha utoaji mikopo ya dharura cha Benki ya taifa ya Ethiopia, NBE, ambacho benki hutumia wanapokabiliwa na matatizo kitaongezwa kutoka 16% hadi 18%.
Kwa mwaka huu wa fedha wa Ethiopia unaokwishia Juni 30, 2024, ukuaji wa mikopo utapunguzwa hadi asilimia 14 na benki zote za biashara zitaelekezwa kupunguza mikopo ili kuendana na ukomo huu wa jumla wa mikopo.