Eneo la Tigray kaskazini mwa ethiopai lina jamii ya Wakristu na waislamu /  Picha: AP

Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia limetoa ilani ya siku tatu kwa serikali kutoa maagizo ya kuwakataza watoto wa kike kuvaa hijab wakiwa shule.

"Ikiwa ombi letu halijajibiwa ndani ya siku tatu, tunaweza kuchukua hatua zaidi za amani kwa kushauriana na waumini.”

Wanafunzi wa dini ya Kiislamu katika mji wa Axum, ulioko katika Ukanda wa Kati wa eneo la Tigray, wanapinga marufuku ya hijabu ambayo wanasema imewazuia kuhudhuria shule na kukiuka haki zao za kikatiba za elimu na uhuru wa kidini.

Katika barua ya tarehe 10 Oktoba, 2024, Ofisi ya Masuala ya Kiislamu huko Axum hapo awali ilizitaka shule kuheshimu haki za kidini za wanafunzi wa kike wa Kiislamu.

Barua hiyo ilisisitiza kwamba kuvaa hijabu ni wajibu wa kidini na iliangazia kuwa marufuku hiyo inaathiri shule nne za sekondari—Woree, Kindeya, Adebabay na Messenado. Takriban wanafunzi 140, wakiwemo wanafunzi wa darasa la 12 waliripotiwa kunyimwa usajili wa mitihani ya kitaifa.

Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Tigray linasema viongozi wa shule hawapaswi kupingana na katiba kwani Wizara ya Elimu inaruhusu kuvaa kwa hijab.

Vita kaskazini mwa Ethiopia kati ya 2020 hadi 2022 vilifanya watoto kukosa kwenda shule / Picha:  AP

"Ni kinyume cha sheria na si haki kuwaweka wanafunzi wetu wa kike Waislamu mbali na shule kwa miaka mitatu kutokana na vita, kwa sababu tu wanavaa hijabu inayoakisi utambulisho wao. Tunaomba hili litatuliwe mara moja kwani linadidimiza umoja wetu," taarifa imeongezea.

"Mgogoro wa kisiasa na mazingira huko Tigray unatosha. Kufungua mlango kwa mzozo unaoegemezwa kwenye dini kutasababisha eneo hilo kutoka katika hali mbaya zaidi," viongozi hao wa dini wameonya.

Changamoto jijini Addis Ababa

Katika mji mkuu wa Addis Ababa, changamoto hiyo pia imeshuhudiwa.

Mwaka uliopita wanafunzi Waislamu walisimamishwa katika shule nne za sekondari kwa kuvaa niqab, huku viongozi wa shule wakishutumiwa kwa "shinikizo na unyanyasaji.

Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu la Addis Ababa lililaani kitendo hiki kama "kutowajibika" kwa shule hizo na kukosa uhalali wa kisheria.

Baada ya makubaliano na maafisa kutoka Ofisi ya Amani na Usalama ya Addis Ababa, Polisi wa jiji, na Ofisi ya Elimu wanafunzi walikubaliwa kuvaa kulingana na dini na kuendelea na masomo.

Na sasa viongozi wa Kiislamu katika eneo la Kaskazini mwa nchi wanataka uamuzi kama huo.

"Tunaomba jumuiya ya Kiislamu na wengine wanaotafuta amani waadilifu na Wakristo ambao wanashiriki kwenye mitandao ya kijamii kuweka shinikizo katika kuondolewa kwa marufuku ya hijab. Elimu ni mojawapo ya haki za msingi za binadamu," wameongezea katika taarifa yao.

TRT Afrika