Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman amejiuzulu.
"Leo, nilitangaza kwa timu yangu katika ubalozi wa Marekani kwamba niliwasilisha barua yangu ya kujiuzulu kwa Rais Biden," alisema katika taarifa.
"Nitaondoka Kenya nikiwa nimejawa na shukrani kwa timu ambayo imefanya kazi bila kuchoka kwa niaba yangu, kwa fursa ya kutumikia nchi yangu, na kwa urafiki unaotolewa na serikali na watu wa Jamhuri nzuri ya Kenya, " ameongezea.
Kujiuzulu kwake kunakuja siku chache baada ya mgombea wa chama cha Republican Donald Trump kushinda kiti cha urais.
Aliteuliwa kushika wadhifa huo na Rais anayeondoka madarakani Joe Biden mnamo Disemba 2021. Alithibitishwa Julai 2022 na kuanza kazi mwezi uliofuata.
Whitman alisema anajivunia kuongoza ajenda inayozingatia watu ambayo iliokoa maisha, kuongeza usalama na kuunda fursa za kiuchumi kwa Wakenya na Wamarekani.
"Kuanzia kutoa ufadhili wa dharura ili kupunguza janga la mafuriko mwaka 2023 hadi vita vinavyoendelea dhidi ya Malaria, Ukimwi na MPOX. Serikali ya Marekani inaweka mbele afya na ustawi wa marafiki zetu nchini Kenya, " Whitamn amesema katika taarifa.
"Mwaka huu, Marekani iliinua Kenya kama mshirika wake mkuu wa kwanza asiye wa NATO katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikionyesha umuhimu ambao nchi zetu zinaweka katika kusimama bega kwa bega maadili yetu ya pamoja ya kidemokrasia na kuimarisha usalama."
Alisema juhudi zake zimefungua milango kwa kampuni nyingi za Kimarekani kufanya biashara nchini Kenya na hii imeongeza biashara, ajira na uwekezaji wa Marekani nchini Kenya.
Whitman alibainisha kuwa, kama ilivyo kwa mabalozi wote, anahudumu kutokana na ombi la Rais, na sasa rais mpya atakuwa akichukua uongozi wa Marekani, yaani Donald Trump, kuanzia 2025.